SERIKALI YAEKEZA ZAIDI YA SH. BILIONI 32 KIBONG’OTO KUBORESHA HUDUMA ZA MAGONJWA AMBUKIZI
Posted on: February 21st, 2026Na WAF, Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto imepokea zaidi ya shilingi bilioni 32 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fedha zilizolenga kuboresha miundombinu na huduma za afya hususan za magonjwa ambukizi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika hospitali hiyo, Dkt. Samizi amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 8 zimetumika kujenga jengo la radiolojia litakalosaidia kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya wagonjwa.
Dkt. Samizi amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutokomeza magonjwa ambukizi ikiwemo kifua kikuu (TB) ifikapo mwaka 2030, ambapo tayari hatua zimechukuliwa kuboresha tiba na huduma za ugunduzi wa mapema.
Ameeleza kuwa kwa sasa wagonjwa wa TB sugu wanatibiwa kwa muda mfupi zaidi wa miezi tisa badala ya miezi 11 hadi 18, huku wagonjwa wa TB wa kawaida wakitibiwa kwa muda usiozidi miezi tisa. Hatua hiyo inalenga kuwezesha wagonjwa kupona haraka na kupunguza madhara ya ugonjwa huo katika jamii.
“Hatungojei wagonjwa wafike hospitalini pekee, Serikali imeimarisha huduma za uchunguzi wa TB kwa njia ya mobile clinics ili kuwafikia wananchi moja kwa moja kwenye jamii na kuwapatia matibabu mapema,” amesema Dkt. Samizi.
Aidha, amesema Serikali imerudisha na kuimarisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa lengo la kuwagundua wagonjwa wa TB mapema na kuwasaidia kupata huduma stahiki kwa wakati, huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za afya wanapohisi dalili zozote.
Katika hafla hiyo, jiwe la msingi limewekwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambapo Dkt. Samizi amewataka wachimbaji wa madini nchini kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yanayohusiana na shughuli za uchimbaji, ikiwemo maradhi ya silicosis ambayo hayana tiba.