SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA NICU KWIMBA, JENGO LA KWANZA LA HUDUMA KUZINDULIWA MACHI 1, 2026.
Posted on: February 18th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Mwanza
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Afya imeendelea kuboresha huduma za Afya ya Uzazi, mama na mtoto kwa kujenga jengo jipya la huduma za watoto wachanga na waliozaliwa kabla ya wakati (NICU) hatua inayolenga kupunguza kwa kasi vifo vya mama na mtoto katika maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Watoto Wachanga, Watoto na Vijana Dkt. Felix Bundala, Februari 16, 2026 wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa jengo jipya la NICU lilifadhiliwa na Taasisi ya Doris Mollel, linalotarajiwa kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Machi Mosi, 2026, wilayani Kwimba, Mwanza.
Dkt. Bundara amesema kuwa jengo hilo la NICU ni la kwanza nchini kujengwa kwa viwango vya kimataifa na kuongeza kuwa litaanza kutoa huduma kwa wananchi kabla ya uzinduzi.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza mapambano ya kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kasi zaidi, hatua inayothibitisha dhamira ya Rais Samia katika kuimarisha afya ya mama na mtoto, ikiwa ni pamoja na kutambuliwa kwake kimataifa kwa juhudi hizo.
“Pia timu ya madaktari bingwa na bobezi wa watoto wako hapa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watoa huduma wa kituo hicho, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika mapema na uwekezaji huo muhimu katika sekta ya afya ya mama na mtoto,” amesema.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kwimba Mhe. Ngw’ilabuzu Ludigija amesema mradi huo umeletwa katika eneo sahihi kutokana na changamoto za vifo vya mama na mtoto zinazochangiwa na baadhi ya jamii kutojifungulia katika vituo vya afya na kuendelea kutumia waganga wa jadi,
Aidha, ameeleza kuwa hospitali hiyo pia inapokea wagonjwa wa rufaa kutoka mikoa ya jirani ikiwemo Shinyanga, jambo linaloongeza mahitaji ya huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Dori Mollel, Bi. Doris Mollel ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa katika kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, akieleza kuwa mradi huo umefanikiwa kwa misingi ya ushirikiano wa timu, huku wafadhili wa ziada ameonesha nia ya kuongeza ufadhili ili kujenga majengo mengine ya huduma za afya.
“Sambamba na ujenzi wa jengo hilo pia kumejengwa nyumba za watumishi. Matamanio yangu ni kuwepo na huduma za ziada kama vile wataalamu wa msaada wa kisaikolojia kwa wazazi wanaopata watoto njiti hili litasaidia kwa wakina mama hao afya za akili zao,” amesema Bi. Doris