Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

AFUA ZA CHANJO NCHINI KUZIDI KUPEWA MSUKUMO KWA MASLAHI YA UMMA

Posted on: February 20th, 2026

Na Happynes Hans, WAF - ARUSHA


Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga na Mpango wa Taifa wa Chanjo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na wadau wa sekta ya afya, inaendelea kutekeleza afua za utoaji na uhamasishaji wa huduma za chanjo nchini ikiwa ni mpango wa kuzidisha msukumo kwa maslahi ya jamii


Hayo yamesemwa na Afisa Programu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bi. Lotalis Gadau, leo Februari 20, 2026, jijini Arusha, wakati wa kikao kazi cha kukamilisha rasimu ya Mkakati wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma kuhusu Huduma za Chanjo.


Bi. Gadau amesema Mkakati wa Mawasiliano wa Chanjo una mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi, kuondoa hofu na mashaka, na kuhamasisha matumizi ya huduma za chanjo. 


Amesema mkakati huo husaidia kujenga imani kwa mfumo wa afya, kuchochea mabadiliko chanya ya tabia, na kufikia makundi magumu ndani ya jamii kupitia vyombo vya habari kama redio, mikutano ya kijamii na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs).


“Mkakati wa mawasiliano wa chanjo utawawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu aina na umuhimu wa chanjo, na kupunguza upotoshaji, hofu na mashaka yanayotokana na uvumi au imani potofu,” amesema Bi. Gadau.


Ameeleza kuwa Wizara ya Afya ina jukumu la kitaifa la kuboresha huduma za chanjo kwa kutunga sera, miongozo na mikakati; kuratibu Mpango wa Taifa wa Chanjo; kufuatilia usalama wa chanjo (AEFI) pamoja na kujenga uwezo wa watoa huduma za afya katika mawasiliano rafiki kwa jamii.


Naye Msimamizi wa Chanjo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bi. Rosalia Arope, amesema TAMISEMI ni kiungo muhimu kati ya sera za kitaifa na utekelezaji wake ngazi ya jamii.


"TAMISEM inasimamia utekelezaji wa huduma za chanjo katika mikoa na halmashauri, kuratibu huduma ngazi ya mkoa na wilaya, kuhamasisha viongozi wa mitaa, pamoja na kuwezesha mikutano ya kijamii na kampeni za uhamasishaji, hivyo, TAMISEMI huhakikisha mkakati wa mawasiliano unawafikia wananchi moja kwa moja" amesema Bi. Arope 


Kwa upande wake Mratibu wa Mabadiliko ya Tabia za Kijamii kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumba, amesema UNICEF ina mchango katika sekta ya afya kwa kutoa msaada wa kifedha na kitaalamu kwa programu ya chanjo, kuendeleza mikakati ya mawasiliano inayolenga jamii (SBCC na RCCE), kufanya tafiti za kubaini sababu za baadhi ya wananchi kusita au kukataa huduma za chanjo.