WAZIRI MHAGAMA AWASIHI WAUMINI PERAMIHO KUPIMA AFYA ZAO
Posted on: April 20th, 2025
Na WAF - Peramiho, Ruvuma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo tarehe 20 Aprili 2025, amewasihi waumini wa Kanisa la Kigango cha Liula Parokia ya Matimira, Peramiho mkoani Ruvuma kutumia fursa za uwepo wa Madaktari Bingwa mkoani Ruvuma kupima afya zao pamoja na kusherehekea sikukuu ya Pasaka.
Akizungumza baada ya ibada hiyo, Waziri Mhagama amewataka waumini na wananchi wa Peramiho na mkoani kwa ujumla kuchangamkia fursa ya ujio wa madaktari bigwa wanaotoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya saratani katika hospitali ya MT - Joseph Peramiho.
"Ninawaomba sana, kesho ni siku ya mwisho, naomba muende wakina baba kwa kina mama, ni baraka kubwa sana kupata hii nafasi na ni maelekezo aliyonielekeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ndio zawadi kubwa ya Pasaka kwa wananchi wa pembezoni kwakuwa wengi hawafikiwi na matibabu haya," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, huduma hizo zinatolewa na wataalam bingwa kutoka katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) tena bila malipo na Serikali inajipanga tena kuwaleta madaktari wengine wa moyo ili na wananchi wenye matatizo hayo nao wapate matibabu.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafikiria kushirikiana na Hospitali ya MT - Joseph Peramiho kwa kuanzisha kituo kingine cha tiba ili kuwapunguzia wananchi wa Peramiho na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kwenda kutibiwa Dar es Salaam.