WATUMISHI VITUO VYA AFYA NGAZI YA MSINGI KUPEWA KIPAUMBELE 'SAMIA SCHOLARSHIP'
Posted on: April 9th, 2025
Na. WAF, Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kutoa kipaumbele kwa watumishi kutoka vituo vya Afya ngazi ya msingi kwa kuwapeleka kusoma utaalam wa kibingwa na ubobezi ili kuendelea kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi.
Waziri Mhagama ameyasema hayo Aprili 9, 2025 wakati wa kufunga Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.
“Rais Dkt. Samia ametoa mfuko maalum wa kusomesha wataalam katika sekta ya afya ujulikanao kama Samia Scholarship, hivyo ni lazima tusomeshe kwa seti yaani daktari, mtaalamu wa usingizi, mtaalam wa maabara, na wauguzi tusiwaache nyuma, hivyo tunapoamua kuwapeleka watumishi wa afya kusoma hawa watumishi kutoka vituo vya afya vya msingi wapewe kipaumbele kwa sababu hawa ndio wanaotoa huduma ya matibabu kwa asilimia 80, hivyo ni vyema kupeleka huduma za kibingwa na bobezi ngazi ya msingi,” amesema Mhe. Mhagama
Waziri Mhagama amewataka waganga wafawidhi kuwa mfano wa kuigwa kwa maadili mema na kuwasimamia vizuri watumishi wanaowaongoza ili kuhakikisha kwa pamoja sekta ya Afya inapata heshima kwa kufuata viapo walivyoapa, miongozo na maadili.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tamisemi wako mbioni kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kugawa vishikwambi 600 na kwa waganga wafawidhi ili kuendana na kasi ya ulimwengu wa dijitali.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Wizara ya Afya inatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia ya kupeleka kiasi cha Shilingi Bilioni 1 ofisi ya Rais Tamisemi ili kusaidia kufikisha mfumo wa usimamizi katika maeneno ambayo haujafika.
“Niwaombe sana Waganga Wafawidhi kusimamia mifumo ya matumizi, usimamizi na uendeshaji wa vituo vya afya ngazi ya msingi hasa wa mapato,” amesema Mhe. Mhagama.