Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI 108 SEKTA YA AFYA WAPIGWA MSASA KUKABILIANA NA DHARURA ZA UZAZI

Posted on: April 19th, 2024



Na WAF- Mara

Watumishi 108 wa Afya kutoka kwenye vituo vya Afya vipatavyo 25 kati ya 37 vinavyotoa huduma ya upasuaji wa mtoto, mkoani Mara wamejengewa uwezo maalum kwa ajili yakukabiliana na dharura za uzazi pindi zitokeapo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema kuwa mafunzo watakayopewa watumishi hao ni msisitizo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Dkt. Magembe ameyasema hayo Aprili 19, 2024 alipokuwa akifungua Mafunzo ya kukabiliana na dharura zitokanazo na uzazi Mkoa wa Mara.

“Haya mafunzo yanakuja kufanyika kwenu nyinyi watumishi wa afya ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na dharura za uzazi kwasababu kinacho tutofautisha sisi watumishi wa sekta ya afya na sekta nyingine ni suala la dharura kumsaidia mama kurudi katika hali yake pale anapopata changamoto ya uzazi” Amesema Dkt. Magembe

Dkt. Magembe amesema huo ni mwanzo lakini shabaha nikuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika nchi nzima hasa kwenye vituo vinavyotoa huduma ya wajawazito kujifungua.

Katika hatua nyingine Magembe amesema mbali ya kuwapatia mafunzo pia itafanyika tathimini na ufuatiliaji wa mafunzo hayo kwa njia tehema ili kuwezesha kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Msatu amesema kuwa kupitia mafunzo haya yatawezesha kupunguza vifo vya mama na mtoto na kufikia malengo ya kitaifa na kidunia ambayo yamewekwa kwa kuhakikisha wanaongeza ujuzi kwa watumishi ili kuongeza ujuzi katika vituo takribani 37 vya kutoa huduma za dharura ndani ya Mkoa wa Mara.

Kulingana na Takwimu za Januari hadi Disemba 2023, kati ya wajawazito 103,478 waliojifungua kwenye vituo 344 vya Mkoa wa Mara, 42,444 sawa na asilimia 41%, walijifungua kwenye vituo hivyo 25 vya CEmONC vilivyochaguliwa, ambapo ninyi washiriki wa mafunzo haya mnafanya kazi.

MWISHO