WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA PAMOJA ILI KUBORESHA HUDUMA ZA DAMU SALAMA
Posted on: October 16th, 2025
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kuwa ushirikiano kwenye utekelezaji wa majukumu kati ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Mikoa na Halmashauri ni nguzo muhimu katika kurahisisha utendaji kazi na hivyo kuongeza ufanisi kwenye upatikanaji wa damu salama kwa wananchi.
Dkt. Magembe ameyasema hayo Oktoba 15, 2025 alipotembelea na kuzungumza na watumishi wa Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Ziwa, Jijini Mwanza ambapo pia alikagua maabara na chumba maalum kwa ajili ya wachangia damu.
"Ushirikiano wa Mpango wa Damu Salama, Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kutapelekea kupanga mikakati thabiti ya kuimarisha huduma za damu salama ikiwemo kuongeza wigo wa wachangiaji na kutatua changamoto zinazojitokeza"
Katika hatua nyingine amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya, imeagiza mashine kubwa zaidi mbili aina ya Alinity s zenye uwezo wa kutoa majibu 600, sawa na sampuli 150 za damu kwa muda wa saa moja tu.
Aidha Dkt. Magembe amesema, Wizara ya afya kwa kushirikiana na mkoa, tayari wameshawapangia wataalam wengine watano (5) kuhamia kituo hicho kwa lengo la kuimarisha huduma hizo za damu salama.
Sambamba na hilo, Dkt. Magembe amekutana na kuwapongeza wanachi ambao ni wachangiaji wa muda mrefu wa damu na kuwaomba kuendelea kuwa kielelezo chanya katika uokoaji wa maisha ya watu wenye uhitaji wa damu salama hususani waathirika wa ajali, mama wajawazito na watoto.
Kwa upande wake Meneja Mpango wa Damu Salama Dkt Abdu Bhombo ameishukuru Wizara kwa kuongeza kiwango cha bajeti inayotengwa kwa ajili ya huduma za damu salama ambapo fedha hizo zimeongezwa kwa zaidi ya asilimia 50 na kwamba ongezeko hilo limechangia kuongeza timu za ukusanyaji wa damu na kuwezesha Mpango wa Damu Salama kuboresha huduma zake ikiwemo Kanda ya Ziwa.
"Tukuahidi Mganga Mkuu wa Serikali tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa weledi zaidi na kuwa wabunifu ili kukuza na kuboresha utoaji wa huduma ya Damu Salama.