WATAALAM WA MAABARA WAJENGEWA UWEZO KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO
Posted on: September 14th, 2026Na Zakayo Mosha - WAF MWANZA
Wizara ya Afya kupitia Idara ya huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), inaendesha mafunzo kwa Wataalam wa Maabara wa vituo vya umma na binafsi kutoka Mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Tanga, Kilimanjaro, Singida na Mara kwa lengo la kuwajengea uwezo na utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko nchini.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya Mafunzo hayo leo Septemba 14, 2026 Jijini Mwanza, Mratibu wa huduma za Maabara sehemu ya uchunguzi, ufuatiliaji na uthibiti wa Magonjwa (Laboratory-Based Surveillance and responce) kutoka Wizara ya Afya Bw. Joakim Chacha amesema, mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tano kuanzia Septemba 14-18,2026.
Aidha, ameeleza kuwa, mafunzo hayo yameanza leo na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi siku ya Jumanne Septemba 15, 2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Bw. Chacha amesema kufanyika kwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Afya hapa nchini ambayo yanatolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mradi wa "Pandemic Fund".
"Ni mategemeo yetu kuwa jumla ya Washiriki 42 kutoka Mikoa 7 wa vituo vya Umma na Binafsi kwa ngazi za Mikoa na Msingi watajengewa uwezo wa namna bora ya uchukuaji, ukusanyaji,uchakataji na usafirishaji salama wa sampuli za magonjwa ya mlipuko kwa lengo la kuimarisha usalama wa watumishi wa Afya na Wananchi," amesema Bw. Chacha.
Kwa upande mwingine mshiriki wa mafunzo hayo Bw. Eustadius Kamugisha Mtaalamu wa Maabara kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba ambaye pia ni mbobezi wa utafiti na ufuatiliaji wa magonjwa na usimamizi wa Maabara, ameishukuru Wizara ya Afya na Shirika la Afya duniani (WHO) kwa kuendelea kuweka umuhimu wa mafunzo kwa Wataalam wa Maabara.
"Sisi Wataalam wa Maabara tunaomba mafunzo kama haya kuendelea kutolewa kwa Wataalam wengi zaidi, kwani Wataalam wa Maabara wanaongozwa na tafiti na taarifa sahihi zinazosaidia kufanya maamuzi ya utoaji wa huduma bora za afya kwa Wananchi" amesisitiza Bw. Kamugisha.