Wizara Ya Afya

WATAALAM WA MAABARA WAHIMIZWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI

Posted on: September 11th, 2026

Na Zakayo Mosha- WAF Morogoro

Wataalam wa Maabara wamehimizwa kutumia vema ujuzi na maarifa waliyoongezewa katika mafunzo ya siku tano waliyopata Mkoani Morogoro ili kuboresha utoaji wa huduma bora za vipimo kwa Wananchi mbalimbali wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Wito huo umetolewa leo Septemba 11, 2026, Mkoani Morogoro na Bw. Joakim John Chacha Mratibu wa Huduma za Maabara sehemu ya Uchunguzi, Ufuatiliaji na Uthibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku tano kwa Wataalam wa Maabara kutoka katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Morogoro.

Amesisitiza Wataalam hao, kutumia mafunzo waliyopata kama chachu ya kutoa majibu sahihi ya vipimo na kwa wakati ili yasaidie katika utoaji wa maamuzi ya matibabu kwa wagonjwa.

"Kwa kuwa mmejengewa uwezo wa namna ya ukusanyaji, usafirishaji na uchakataji wa sampuli kwa njia zilizo bora na sahihi, naomba mtimize wajibu wenu na kuwashirikisha wenzenu katika vituo vya kazi ili kutimiza lengo la Serikali yetu la kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora za Afya kwa Mwananchi," amesema Bw. Chacha.

Aidha, ameongeza kuwa hadi sasa jumla ya Wataalam 162 kutoka Mikoa 17 wamepatiwa mafunzo na kujengewa uwezo katika Ufuatiliaji wa Magonjwa (Laboratory-Based Surveillance), amesema hizi ni juhudi za Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Naye Bw. Robert Makala Mwenyekiti wa Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Mikoa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, amesema mafunzo hayo yametolewa wakati muafaka ambapo mamlaka ya Hali ya hewa nchini imetangaza kutakuwa na mvua nyingi, amewataka Wataalam wa maabara kujiandaa vema kukabiliana na madhara yoyote yatakayotokana na mvua hizo ikiwemo Magonjwa ya mlipuko kama vile Magonjwa ya tumbo na kipindupindu.