Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAM ARUSHA WAVUNA MAARIFA KWA MABINGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: May 13th, 2025

Na WAF, ARUSHA 


Madakatari Bingwa wa Rais Samia wameendelea kuwa gumzo miongoni mwa wataalam wanaowajengea uwezo kwenye ngazi za msingi huku wakiipongeza Serikali kwa mpango huo unaookoa maelfu ya afya za Watanzania. 


Hayo yamebainishwa wakati wa zoezi la kuwasogezea wananchi huduma sambamba na kuwajengea uwezo wataalam katika vituo vya mkoani Arusha Mei 13, 2025, zoezi linaloendelea kwenye halmashauri zote saba za mkoa huo.


"Hapa sisi tupo  19 tumepewa maelekezo na Mamlaka ya Mganga Mkuu wa Jiji kuwa, tushiriki kwenye zoezi hili, ili tuweze kuvuna ujuzi na maarifa kwa mabingwa hawa na tutakaporejea kwenye vituo vyetu tuongeze tija," amesema  Dkt.Nkinda Charles  kutoka kituo cha Afya Levolosi cha jiji la Arusha.


Kwa upande wake Bw. Kelvin Mwanga tabibu wa  Kituo cha Afya Ngarenaro, aliye chini ya usimamizi ya Daktari Bingwa wa watoto  Dkt. Anna Magembe, amesema  ndani ya siku moja amenufaika na Madaktari Bingwa hao kufuatia tatizo la mtoto aliyefika kwenye matibabu akiwa na tatizo kubwa na kuongozwa na msimamizi wao hatua zote muhimu wakati wakuchukua maelezo ya mgonjwa.


Akizungumzia mwenendo wa kambi hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya jiji la Arusha Dkt. Samia Kitara, amesema wamefanikiwa kuwaona wananchi wenye changamoto ya afya wapatao 200 ndani siku mbili.


"Tunajua hawa wakishapata huduma na kurejea makwao watakuwa mabalozi wetu, kwani tulihamasisha kwa matangazo ya njiani  lakini pia nyumba za ibada na maeneo ya masoko juu ya ujio wa Madaktari Bingwa na Bobezi," amesema Dkt. Kitara.


Nao baadhi ya Wananchi waliofika kupata huduma wamesifu huduma ya X Ray ya Kisasa ambayo imewarahisishia huduma lakini pia kupunguza umbali wa kwenda kufuata huduma mjini.


"Kabla tulilazimika kwenda kituo cha afya Kaloleni, ambapo awali kilitumika kama Hospitali ya jiji na kama shida ilikuwa kubwa tuliandikiwa kwenda Mount Meru, lakini sasa huduma tunaipata hapa hapa, nampongeza sana Raisa Samia," amesema  Bw. Lamesia Ole Purukwa mkazi wa Njiro Kontena jijini Arusha.


Jopo la Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia Suluhu Hassan wapo mkoani Arusha kwa ajili ya huduma za kibingwa kwa muda wa siku sita kwenye halmashauri zote saba (7) za mkoa huo.