WANANCHI ZAIDI YA 1000 KUFANYIWA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO MBEYA
Posted on: May 14th, 2025
NA WAF – MBEYA
Wananchi zaidi ya 1000 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kupitia kambi maalum ya matibabu ya macho.
Hayo yameelezwa leo, Mei 14, 2025, na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Catherine Nyema katika kambi ya matibabu ya mtoto wa jicho inayoendelea mkoani Mbeya.
Katika Kambi hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Helen Keller, na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dkt. Nyema amesema lengo ni kuondoa ulemavu wa kutokuona na kuwarejeshea wananchi uwezo wa kuona.
“Tunataka kuona jamii inayoweza kufanya kazi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” amesema Dkt. Nyema.
“Ili kuwafikia wahitaji kwa ufanisi, tumetumia mbinu ya kuwafuatilia kaya kwa kaya kwa msaada wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii. Njia hii imewezesha kuwabaini wananchi wengi waliokuwa wakihitaji matibabu lakini hawakuwa na taarifa sahihi. Ushirikiano wa karibu na jamii umeongeza ufanisi wa zoezi hili,” ameongeza Dkt. Nyema.
Aidha, amesema kuwa kupitia uchunguzi uliofanyika, wamegundua jumla ya wagonjwa 1,200 wenye matatizo ya mtoto wa jicho.
“Hii inaonesha ukubwa wa tatizo na umuhimu wa kuendelea na huduma hizi za kambi. Wagonjwa hawa sasa wana matumaini ya kurejesha uwezo wao wa kuona,” amesema Dkt. Nyema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Helen Keller, Dkt. George Kabona, amesema mwaka huu wamepanga kuwafikia wananchi zaidi ya 3,000 katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa na Songwe.
“Matibabu haya yote ni bila malipo, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma za macho, ”amefafanua Dkt. Kabona.