Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA FURSA YA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: May 20th, 2024



Na WAF – Kilimanjaro.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi na kutumiua fursa ya kambi za madaktari bingwa wa Rais Samia kwenye hospitali za wilaya za mkoa ili kujua afya zao na kupatiwa matibabu ya kibingwa.

Mhe. Babu ameyasema hayo Mei 20, 2024 wakati akiwapokea na kuwakaribisha madaktari bingwa wa Rais Samia katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro watakaoweka kambi kwa siku tano na kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi ngazi ya wilaya sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.

“Wananchi wa Kilimanjaro mnabahati sana, hivyo mtumie fursa hii ya kuwa na madaktari bingwa hawa ndani ya siku tano mkapime afya zenu na kupata matibabu na ushauri juu ya changamoto zitakazokuwa zinawakabili kupitia madaktari bingwa wa Rais Samia”. Amesema Mhe. Babu

Aidha, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwamuzi wake wa kuwatuma madaktari bingwa kwenda kwenye halmashauri zote nchini kutoa huduma za kibingwa karibu na wananchi.

“Wananchi wetu sio wote wenye uwezo wa kufuata huduma za kibingwa katika hospitali za kanda na Taifa hivyo tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwatumia madaktari bingwa na kufikisha huduma kwa wananchi wa ngazi ya chini kabisa, Imani yangu kwenu mtatoa huduma za kibingwa kwa wananchi wetu wa mkoa wa Kilimanjaro dhidi ya matatizo waliyokuwa nayo, Karibuni sana mkoa wa Kilimanjaro na ninaahidi ushirikiano wangu muda wote.” Amesema

Wakati huo huo Mhe. Babu amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kujenga hospitali mpya za kila wilaya na kujengwa kwa jengo la kina mama na mtoto katika hospitali ya rufaa ya mawenzi na limepagwa kuanza kazi hivi karibuni.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya ya mama na mtoto Wizara ya Afya Dkt. Mzee Nassor amesema lengo la kambi hizo za Madaktari bingwa wa Rais Samia ni kuwafikia wananchi katika vituo vya afya ngazi ya msingi na kuwaondoshea gharama za matibabu na kupunguza rufaa pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari wengine walio kwenye hospitali za wilaya za mikoa.