WANANCHI ULYANKULU WAMPA KONGOLE RAIS SAMIA ZOEZI LA MADAKTARI BINGWA
Posted on: April 30th, 2025
Na WAF, Tabora
Wanachi wilayani Kaliua mkoani Tabora katika kituo cha Afya Ulyankulu wamepongeza hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwapelekea huduma ya Madaktari Bingwa kwenye kituo Chao.
Pongezi hizo za wananchi zimetolewa Aprili 30, 2025 ikiwa ni siku pili ya kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia katika eneo hilo ambalo limekuwa na uhitaji wa muda mrefu.
"Mara zote tumekuwa tukisikia kambi hii ya wataalam wetu wakija wilayani, lakini walikuwa hawajawahi kufika huku kwetu, hivyo tulikuwa tunashindwa kufika kwa sababu hatuna fedha za kwenda huko," amesema Bw. Slivesta Bahite mkazi wa kijiji cha Ikonongo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya Dkt. Leonard Nyigo amesema, ndani ya siku mbili za huduma wananchi zaidi ya 200 wamejitokeza kwa ajili yakupata huduma za kibingwa.
Dkt. Nyingo ameongeza kuwa, wataalam hao wamekuwa msaada mkubwa sio tu kwa ajili ya huduma lakini pia kuwajengea uwezo watumishi wa Kituo hicho, lakini pia kuanzishwa kwa huduma.
"Tumenufaika na ujio huu, kwakuwa umetuwezesha kuimarisha huduma zetu kama vile huduma ya NCU ambayo ilikuwa haijaanza lakini tulikuwa na vifaa, hivyo tunaishukuru sana Serikali kwa kuona umuhimu," amesema Dkt. Nyigo.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Watoto Dkt. Amos Charles amesema, imekuwa tofauti sana na kambi zingine alizowahi kushiriki kwani ndani ya siku moja tu aliweza kuhudumia watoto 39 kwani kwa kawaida huhudumia watoto kati ya 15 hadi 20 wakati wa Kliniki zingine.
Aprili 28, 2025 Waziri wa Afya Mhe Jenista Mhagama alizindua mzunguko wa tano wa Kambi za Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwaomba viongozi wa ngazi zote kuhamasisha wananchi kujitokeza ili kupatiwa huduma hiyo iliyobuniwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.