WANANCHI TABORA WAJITOKEZA KWA WINGI KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA
Posted on: May 9th, 2025
Na WAF - TABORA
Mratibu wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete, Dkt. Patrick Bilikundi, amesema kumekuwa na muitikio mkubwa wa wananchi katika kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia kwa wananchi kufika na kupatiwa matibabu mbalimbali.
Dkt. Bilikundi ameyasema hayo hospitalini hapo Mei 09, 2025, ikiwa ni siku ya nne ya kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia, ambao wameendelea kutoa huduma mbalimbali za kitabibu.
“Zaidi ya wananchi 2000 wamejitokeza ndani ya siku nne, na tunategemea idadi hiyo itaongezeka. Wengi wamekuwa wakihitaji matibabu ya magonjwa ya ndani na huduma za kitengo cha mifupa, huku tukiwa tumefanya upasuaji zaidi ya 100,” amesema Dkt. Bilikundi.
“Hamasa kubwa tuliyopeleka kwenye nyumba za ibada, mbao za matangazo, huduma ya gari ya matangazo iliyozunguka kwenye kata zote ndiyo imeleta mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza,” amefafanua Dkt. Bilikundi.
“Kutokana na jiografia ya mkoa wetu, kuna wakati huduma za kibingwa si rahisi kufikika, hivyo ujio huu kwetu ni jambo lenye tija kwa afya za wananchi wa Tabora,” ameongeza Dkt. Bilikundi.
Aidha, Dkt. Bilikundi ameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, akisema kuwa hatua hiyo inapunguza gharama za usafiri na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za afya kwa urahisi.