Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAKAZI WA MARAMBA WILAYANI MKINGA WAPATA HUDUMA ZA KIBINGWA KWA MARA YA KWANZA

Posted on: May 21st, 2024


Na WAF – Mkinga


Kambi ya Matibabu ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia iliyoko katika Kituo cha Afya cha Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga imeanza kuwa neema kwa wananchi wa Kijiji hicho waliofika kupata huduma mbalimbali za matibabu ya kibingwa kwa mara ya kwanza kituoni hapo.


Kambi hiyo yenye wataalam watano mapema leo tarehe 21 Mei, 2024 imeanza kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Mkinga katika Kituo cha Afya cha Maramba ‘B’ kilichopo Tarafa ya Maramba ikiwa ni kituo cha kwanza katika kuhakikisha wanawafikia wakazi wa Wilaya ya Mkinga na vitongoji vyake pamoja na kuwapa uzoefu wataalam wa Afya wa wilayani humo.


Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Maramba, Dkt. Josephat Mapunda amesema amewapokea Madaktari Bingwa watano ambao ni Daktari Bingwa wa Afya ya Mama na mtoto, Daktari Bingwa wa upasuaji, Mtaalamu wa usingizi salama pamoja na Dakatari wa Magonjwa ya ndani. 


“Ujio wa Madaktari Bingwa hawa umesaidia sana kwa wakazi wa hapa Maramba na Mkinga kwa ujumla katika kupata fursa ya kupata matibabu ya kibingwa moja kwa moja kwenye Vituo vyetu vya Afya badala ya kutumia gharama kwenda Bombo au Muhimbili badala yake wanawaona hapa hapa na sisi kama watumishi tunapata fursa ya kujifunza kutoka kwa hawa Madaktari bingwa na huu ujuzi wanaotuachia sisi utaendelea kuutumia ili kuwasaidia wananchi wetu”. Amesema Dkt. Mapunda.


“Aidha, Dkt. Mapunda amesema Kambi hiyo imekuwa na neema kubwa baada ya kupata ya kupewa ujuzi wa kutumia machine ya (ultrasound) ambayo ilinunuliwa kwa fedha za kituo lakini haikuweza kutumika kwa kukosa mtaalamu mwenye ujuzi.


 “Madaktari bingwa wametupa uzoefu na rasmi wa kutumia machine hii hivyo kuanzia leo itaendelea kutumika mahali hapa, pia tulikuwa na upungufu wa vifaa kama mashine ya kufuatilia mapigo ya moyo (Cardiac Monitor) ambayo ilikua haifanyi kazi, madaktari hawa wameirekebisha na sasa iko vizuri kwahiyo itatusaidia katika kufanya kazi za upasuaji kwa urahisi zaidi”. Ameongeza Dkt. Mapunda.


Mganga Mfawidhi huyo amemshukuru Rais Dkt. SamiaSuluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya Afya nchini kwa kuwezesha miundombinu, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba pamoja kupeleka Wataalam wa afya ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.


Kwa upande wake Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Mount meru Dkt. Harrison Nkya amesema toka wameanza kazi katika kituo hicho wamewaona wananchi zaidi ya 100 wenye matatizo mbalimbali yanayohitaji tiba ya kawaida pamoja na upasuaji.


“Hadi kufikia sasa tayari tumeona Wagonjwa wa aina mbalimbali ambao wamekuja kambini hapa na wengi wao wakiwa ni wenye changamoto ya ngiri, tezi dume, uvimbe kwenye uzazi, mfumo wa upumuaji pamoja magonjwa ya ngozi hivyo tayari tumewaona na kuanzia kesho tumewapangia kufanyiwa upasuaji ambao una uwezekano wa kufanyika hapa na kama kuna uhitaji wa kuwapa rufaa tutafanya hivyo kwa sababu ya mazingira au miundombinu watapelekwa kwenye hospitali kubwa”. Amesema Dkt. Nkya.