WAJAWAZITO ZAIDI YA 20,000 KANDA YA MAGHARIBI WAPATIWA UANGALIZI MAALUM
Posted on: April 15th, 2025
Na WAF - KIGOMA
Mikoa ya Kanda ya Magharibi kwa kushirikiana na Watoa Huduma ya Afya ngazi ya Jamii (CHWs) kwa kipindi cha Mwaka 2024 imefuatilia kwa ukaribu wajawazito zaidi ya 20,000 waliogundulika kuwa na vidokezo vya hatari na kuwapatia uangalizi na huduma maalum ili kujifungua salama.
Hayo yamebainishwa Aprili 14, 2025 mkoani Kigoma kupitia taarifa ya utekelezaji kutokana na maazimio ya kikao cha Afya ya Uzazi na Mtoto cha kanda ya Magharibi kilichofanyika Januari 20, 2023.
Taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mratibu wa Kanda ya Magharibi wa huduma za Mama na Mtoto Bw. Emanueli Amsi, wakati wa mkutano wa mwaka wa tathmini wa huduma za afya ya uzazi na mtoto Kanda ya Magharibi.
Taarifa imebainisha katika mkoa wa Katavi jumla ya akina mama 2994 wamefuatiliwa mwaka 2024 huku mkoa wa Kigoma Wajawazito 17,026 waliogundulika kuwa na vidokezo vya hatari walifuatiliwa na CHWs na wote walipatiwa huduma muhimu na ungalizi uliosaidia kuwavusha salama.
“Mkoa wa Tabora watoa Huduma ngazi ya Jamii wamekuwa wakishirikishwa katika kuwafuatilia wajawazito wote waliogundulika kuwa na vidokezo vya hatari,” amesema Bw. Amsi
Ameongeza kuwa Kanda ya Magharibi pia imefanikiwa kuweka mtumishi (Focal person) wa kufuatilia wajawazito wenye vidokezo vya hatari katika kliniki za Afya ya Uzazi na Mtoto kwa kila kituo cha kutolea huduma za Afya ambapo mkoa wa Katavi una vituo132, Kigoma vituo 289 na Tabora vituo 391.
Awali akifungua mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto, Wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi na watoto wachanga bado bidii na uwajibikaji vinahitajika ili kufikia malengo ya kimataifa na ya kitaifa.