UPASUAJI WA HARAKA WAOKOA MAISHA YA BI. KIARA MKOANI ARUSHA
Posted on: May 22nd, 2024
Madaktari Bingwa wa Mhe. Dkt. Samia wanaoendelea na kambi ya kitabibu Mkoani Arusha katika hospitali ya Wilaya ya Meru, wamefanikiwa kufanya upasuaji na kuondoa uvimbe uliokuwepo zaidi ya miaka 5 kwa Bi. Consolata Kiara mwenye umri wa miaka 54 aliekuwa na tatizo la hedhi isiyokoma.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dkt. Nathan Warioba ameongoza upasuaji huo uliodumu kwa zaidi ya masaa matatu huku akieleza kuwa hali ya mama huyo ilikuwa mbaya alivyofika hospitali kwakua alikuwa na hedhi isiokoma hali iliopelekea kupoteza damu nyingi mwilini na kupelekea kufanyiwa upasuaji wa haraka kuondoa uvimbe huo.
Nae, Bi. Kiara ameelezea hali yake kabla ya upasuaji huo ilikuwa mbaya kwani alikuwa anapoteza damu nyingi ambapo ilikua inapelekea kushindwa kuendelea na shughuli zake za kila siku mpaka pale aliposikia kambi ya kitabibu ya kibingwa ya Madaktari wa Samia na kuweza kufika hospitali na kuhudumiwa kwa haraka
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa Madaktari hao hospitalini hapo kwani hali yake kwa sasa inaendelea kuimarika.
Aidha, mpaka sasa madaktari bingwa wamefanikiwa kufanya upasuaji 7, 4 zikiwa upasuaji wa wamama wajawazito walioshindwa kujifungua kawaida, 1 ikiwa uvimbe kwenye kizazi, 1 uvimbe kwenye shingo na 1 ikiwa ni kuondoa henia kwenye tumbo na wamefanikiwa kuwaona wagonjwa 164 kwa muda wa siku mbili toka kambi imeanza mnamo Mei 20, 2023.
Vilevile, Jopo hilo la Madaktari Bingwa linaendelea kuwajengea uwezo Watumishi wa Afya wa hospitali hiyo ili waweze kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi hali itakayopelekea kupunguza utoaji wa Rufaa kwa Wagonjwa kwenda kutibiwa kwenye hospitali za Rufaa.