Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TARA YATAKIWA KULINDA NA KUTUNZA VIFAA VYA RADIOLOJIA

Posted on: November 5th, 2024

Na WAF-Dodoma

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewahimiza wanachama wa Chama cha Wataalamu wa Radiografia Tanzania (TARA) kuvilinda na kuvitunza vifaa vya radiolojia ili kuleta faida endelevu kwa vizazi vijavyo.

Dkt. Mollel amesema hayo Novemba 04, 2024 Jijini Dodoma alipokutana na Rais wa chama hicho Bw. Bakari Msongamwanja na kutoa maagizo juu ya uboreshaji wa wataalamu wa Radiografia Afrika.

“Ninyi kama TARA mnatakiwa kuhakikisha mnalinda na kutunza vifaa vya radiolojia kwa kuwa ninyi ndio watumiaji wakubwa. Ni muhimu vifaa hivi vidumu kwa muda mrefu ili viwe na matokeo chanya kwa vizazi vijavyo," amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya Bw. Danny Temba amesisitiza umuhimu wa matumizi endelevu na utunzaji wa vifaa hivyo, akibainisha kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hasa uchunguzi wa radiolojia, ikiwemo ununuzi wa mashine za CT scan, MRI, na X-ray na kwamba uwekezaji huu unahitaji uangalizi maalum ili kuhakikisha manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya, Dkt. Saitori Laizer, ametoa wito kwa TARA kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango ya afya na kwamba ushirikiano huu ni muhimu kwa kuwa jukumu la Serikali ni kuwahudumia wananchi na TARA inapaswa kushiriki kikamilifu katika juhudi hizo ili kuleta tija zaidi.

Kwa upande wake, Rais wa TARA, Bw. Msongamwanja, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kupitia radiolojia, akisema kuwa Tanzania kwa sasa ni miongoni mwa nchi nne bora barani Afrika kwa usalama wa radiolojia na kwamba hatua hizo zimeboresha sana huduma za afya nchini.