TANZANIA YAWEKA MAZINGIRA RAFIKI KWA UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA
Posted on: September 3rd, 2026Na John Mapepele – WAF
Washington, D.C.
Serikali ya Tanzania imewaasa wawekezaji wa Marekani na duniani kote kuwa inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji wa sekta ya afya kwa kuweka miundombinu, sera na mifumo ya udhibiti inayolenga kuvutia mitaji na teknolojia.
Hayo yamesema katika Mkutano wa Wadau wa Ushirikiano wa Afya kati ya Marekani na Tanzania mjini Washington, D.C., na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa huku akitaka ushirikiano na kampuni za Marekani unaozalisha thamani ya muda mrefu kupitia uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na ujenzi wa uwezo wa ndani.
"Tanzania ina historia ya ushirikiano wa muda mrefu na Marekani, tukirejea uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na kampuni ya McKinsey & Company mwaka 1970, ambao ulihusisha kusaidia kujenga mifumo ya taasisi za Serikali" amesema Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miundombinu na mazingira ya biashara, ikiwemo upatikanaji wa umeme wa uhakika ambao ni muhimu kwa viwanda vya dawa na bidhaa nyingine za afya.
Katika sekta ya afya, amefafanua kwamba, Serikali imepanua na kuboresha vituo vya huduma nchini kote, huku utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ukitarajiwa kuongeza mahitaji ya dawa, vifaa tiba na huduma za uchunguzi. Amesema uzinduzi rasmi wa Bima ya Afya kwa Wote umepangwa kufanyika hivi karibuni.
Aidha, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha mfumo wa udhibiti wa bidhaa za afya kupitia TMDA, ambayo umefikia Kiwango cha 3 cha shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kuvutia wazalishaji wanaolenga masoko ya kimataifa na kikanda.
Katika hatua nyingine amesema Serikali pia inaendelea kuboresha taratibu za uwekezaji na ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kupunguza vikwazo vinavyoweza kuchelewesha uanzishwaji wa viwanda vya dawa na bidhaa za afya.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa Tanzania haitafuti wawekezaji kwa ajili ya mitaji pekee, bali washirika watakaosaidia kujenga viwanda, kuhamisha teknolojia, kuongeza ajira na kuifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa