Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAUNGA MKONO AZIMIO LA AFYA KWA WOTE NA UBORESHAJI HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA MSINGI KATIKA MKUTANO WA 37 WA JUMUIYA YA MADOLA

Posted on: May 17th, 2025

Na WAF, Geneva Uswisi.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeungana na nchi wananchama wa Jumuiya ya Madola kuendelea kuweka msisitizo wa kufikia lengo la Afya kwa wote pamoja na uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi.


Hayo yamebainishwa leo Mei 17, 2025 na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati akiwasilisha tamko la Tanzania kwenye Mkutano wa 37 wa Jumuiya ya Madola kwenye kikao cha Mawaziri wa Afya kinachofanyika Geneva, Uswisi.


“Tanzania inaendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Madola za kuongoza kasi ya uboreshaji wa huduma za afya kwa wote pamoja na kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi, tunaamini kwa kuwekeza kwenye mifumo ya utoaji huduma za afya tutaweza kufikia malengo endelevu,” amesema Waziri Mhagama.


Waziri Mhagama amesema ili kufikia malengo hayo ni lazima nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuungana pamoja kutekeleza vipaumbele vya kuboresha huduma za afya ili kukabiliana na vikwazo vya ugharamiaji huduma za afya.


Amebainisha kuwa tayari Serikali ya Tanzania imepitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ikiwa ni lengo moja wapo la kufikia afya kwa wote.


“Sheria hii imelenga kuweka mkakati jumuishi na endelevu wa kuendelea kugharamia mifumo ya utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha Watanzania bila ya kujali hali zao za kiuchumi wanapata huduma bora za afya bila ya kuwa na kikwazo cha kifedha,” amefafanua Waziri Mhagama.


Katika hatua nyingine, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Afya Tanzania Bara Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui wamemnadi mgombea wa Tanzania katika uchaguzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani kwa Kanda ya Afrika (Prof. Mohammed Janab) kwa Mawaziri wa Afya na Viongozi kutoka nchi za Bara la Afrika ambao ni wananchama wa Jumuiya ya Madola.