Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: October 16th, 2025

Na WAF – Mwanza

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kudhibiti Magonjwa ya Mlipuko na Dharura za Afya (Pandemic Fund Project), hatua muhimu inayolenga kujenga mifumo imara ya afya, kuimarisha miundombinu ya maabara, na kuongeza uwezo wa kitaalam ili kukabili milipuko kwa wakati.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Oktoba 15, 2025, katika Hoteli ya Malaika Beach, jijini Mwanza, ukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambapo mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Wizara ya Mifugo na Uvuvi na mashirika ya maendeleo ikiwemo WHO, UNICEF na FAO, katika ngazi ya taifa hadi mikoa na wilaya.

Kupitia Pandemic Fund, Tanzania imenufaika na msaada wa Dola za Kimarekani Milioni 25 (takriban Shilingi Bilioni 67), fedha zitakazotumika kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, mafunzo ya wataalam wa afya, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya dharura, pamoja na kuimarisha uratibu wa majibu ya haraka wakati wa milipuko.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Biteko amesema utekelezaji wa mradi huo unaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga taifa lenye uwezo wa kujilinda na kupambana na changamoto za kiafya kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema utekelezaji wa mradi huo utatilia mkazo kwenye kuunganisha mifumo ya afya ya jamii, kuboresha upatikanaji wa taarifa za kiafya kwa wakati, na kujenga uwezo wa ndani wa kushughulikia milipuko kabla haijaenea.

Amesema uzoefu uliopatikana wakati wa kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera, ambao uliweza kudhibitiwa ndani ya kipindi cha chini ya siku 50, ni kielelezo cha uwezo wa wataalam wa afya nchini, na kwamba kupitia mradi huo, mfumo huo wa majibu ya haraka utaimarishwa zaidi.

Dkt. Magembe ameongeza kuwa mradi huo utasaidia kujenga mifumo endelevu ya ufuatiliaji, utambuzi wa mapema wa magonjwa, na ushirikiano wa sekta mtambuka ili kuhakikisha jamii inabaki salama na taifa linakuwa tayari kuka