Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SHILINGI BILLIONI 17 ZA MRADI WA NEST 360 KUBORESHA MIUNDOMBINU NA VIFAA TIBA KWENYE WODI ZA WATOTO WACHANGA NCHINI

Posted on: June 13th, 2024


Na WAF, Dar Es Salaam.


Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya imezindua awamu ya pili ya mradi wa Newborn Essential Solution and Technology (NEST 360), wenye thamani ya Shilingi Bilioni 17 ambao umelenga kuboresha miundombinu ya wodi maalumu ya watoto wachanga katika Vituo vya Afya ngazi ya msingi 21 na kuweka vifaa tiba ili kuimarisha hali ya utoaji wa huduma za Mama na Watoto wachanga nchini.


Mradi huo umezinduliwa leo Juni 13, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Dkt Grace Magembe akimuwakilisha Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambapo hafla ya uzinduzi wa mradi huo imefanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Jijini Dar Es Salaam.


“Tuna furaha kuzindua Mradi huu wa NEST360 ambao ni mwendelezo wa mradi wa awamu ya kwanza uliotekelezwa katika Hopsitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Mkoa Amana, Mwananyamala na Temeke, Hospitali za Kanda Mbeya na KCMC Kilimanjaro. Mradi huu umejikita katika kuboresha huduma za watoto wachanga wakiwemo watoto njiti kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga” ameeleza Dkt. Magembe.


Dkt. Magembe amesema kuwa awamu ya pili ya mradi huo utatekelezwa kwenye vituo 21 vya Afya ya msingi kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Marekani kinachoitwa ‘Rice University’ na Taasisi ya Utafiti ya Ifakara.


Kwa upande wake Rais wa Chuo Kikuu cha Rice, Marekani, Prof. Reginald DeRoche, amesema, mradi wa NEST 360 unatekelezwa Tanzania, Malawi, Kenya na Nigeria na Matokeo ya mradi huo nchini Tanzania yameonesha kuwa makubwa kitu kinachopelekea wao kujivunia.


“Tanzania chini ya Serikali ya Rais Samia imedhamiria kupunguza vifo vya watoto wachanga ili kuendana na Malengo Endelevu ya Milenia na tunaona kazi kubwa inafanyikakuboresha huduma za afya” amesema Prof. Reginald DeRoche.