Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WHO KUIMARISHA MAHUSIANO KURATIBU MAJANGA, DHARURA ZA AFYA YA JAMII

Posted on: November 14th, 2024

Na WAF – Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani ( World Health Organization- WHO), inaendelea kuimarisha ushirikiano na mahusiano yenye lengo la kuboresha uratibu wa majanga na dharura za afya ya jamii nchini lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa mifumo ya afya ya kukabiliana na majanga mbalimbali, ikiwemo milipuko ya magonjwa inayoweza kuathiri afya za wananchi.

Hayo yamebainishwa leo, Novemba 13, 2024, Dkt. Ahmed Makuwani kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, mkoani Dodoma wakati wa zoezi la kupima utayari wa vituo vya operesheni za dharura za afya ya jamii duniani.

“Kupitia ushirikiano huu, tunajitahidi kujenga uwezo wa wataalamu wa afya wa ndani ya nchi kwa kuwapatia mafunzo na vifaa vya kisasa vinavyohitajika wakati wa majanga,” amesema Dkt. Makuwani.

“Hatua hizi ni muhimu ili wananchi wapate huduma za haraka na bora wakati wa dharura, kwani Serikali imeweka mikakati ya kudhibiti mawasiliano ya dharura kwa kuanzisha mifumo ya kiteknolojia ya mawasiliano inayorahisisha utoaji wa taarifa kwa umma na kwa wataalamu wa afya pindi dharura inapotokea,” amesisitiza. Dkt. Makuwani.

Dkt. Makuwani amehitimisha kwa kusema kwamba, Serikali na WHO zinashirikiana kuboresha miundombinu ya afya kama vile vituo vya dharura, mifumo ya upatikanaji wa dawa na usafiri wa haraka kwa majeruhi au waathirika na dharura za kiafya.