SERIKALI, WADAU KUIMARISHA AFUA BUNIFU ZA KUKABILIANA NA UGONJWA WA KIFUA KIKUU
Posted on: November 15th, 2024
Na WAF - DODOMA
Serikali pamoja na wadau wa mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini wameazimia kutekeleza mpango harakishi na shirikishi wa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu na ukoma nchini.
Wakizungumza kwenye kikao cha siku tatu kinachoendelea jijini Dodoma washiriki wa kikao wamebainisha kuwa mpango huu unakuja kwa dharura ili kuziba pengo la wagonjwa ambao hawakuweza kupatikana katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2024 kutokana na sababu mbalimbali, hivyo mpango
huo utakaotekelezwa kupitia kampeni utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapata wagonjwa waliokosekana katika kipindi hicho.
Akizungumza wakati wa majadiliano hayo Mtaalamu Mshauri, Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Emmanuel Matechi amesema mpango huo umelenga kutafuta wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya vyenye idadi kubwa ya wahisiwa wa kifua kikuu.
“Kampeni hii itafikia jamii kupitia watoa huduma wa ngazi ya jamii ambapo wagonjwa na wahisiwa watahudumiwa na pia makundi yote yaliyo katika hatari ya kupata kifua kikuu kama wachimbaji wa madini, wafungwa, wanaoishi na VVU pamoja na watu wanaoishi katika maeneo yenye misongamano yatafikiwa,” amesema Dkt. Matechi.
“Tumejipanga kuyafikia makundi yote yaliyo katika hatari ya kuambukizwa kifua kikuu ili kuwapata wagonjwa wote wa TB na kuwaweka kwenye matibabu na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu sambamba na kufikia malengo ya nchi na ya dunia” ameongeza Dkt. Matechi
Akichangia mada wakati wa Majadiliano, Afisa Kiungo wa kifua kikuu kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bi. Happiness Msengi
amesema elimu inabidi iwafikie wadau muhimu ambao kwa namna moja wana ushawishi ndani ya jamii.
“Tukiwashirikisha viongozi wa dini na wao wakalibeba jambo hili kutokana na wao kuwa na ushawishi, wakiliongea kwenye nyumba za ibada ajenda yetu itafanikiwa” amesema Bi. Msengi
Aidha, akizungumza katika kikao hicho Dkt. Mageda Kihulya kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema kama wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye utekelezaji kila mkoa unapaswa kuwa na ramani ya kazi na namna watakavyo tekeleza.