Wizara Ya Afya

SERIKALI KUTOA SHILINGI BILIONI 3 KUANZA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO KAGERANa Shaban Juma WAF, Dodoma

Posted on: September 2nd, 2026


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni tatu katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.

Dkt. Samizi amesema hayo leo Septemba 02, 2026 Bungeni jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini, Mhe. Eng. Johnston Johansen Mtasindwa, aliyetaka kufahamu lini Serikali itajenga Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.

Amesema Serikali tayari imekamilisha usanifu wa jengo hilo na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi wa ujenzi.

Aidha, Dkt. Samizi amesema ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto unatarajiwa kuanza mapema mwezi Desemba, 2026, hatua itakayosaidia kuimarisha mazingira na upatikanaji wa huduma za afya kwa mama na watoto katika Mkoa wa Kagera.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya nchini kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma bora na za uhakika kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.