SERIKALI KUJENGA VITUO VYA MALEZI NA MAKUZI- DKT. GWAJIMA
Posted on: December 10th, 2021
Na WAMJW – DODOMA
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali inampango wa kujenga vituo vya Malezi na Makuzi kwa ajili yakukabiliana na changamoto ya makuzi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Akizindua programu ya kwanza naya kipekee kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan. Waziri Gwajima, amesema katika miaka ya hivi karibuni, vitendo vya kikatili vimekithiri ndani ya jamii kwa watoto walio na umri mdogo, hivyo ni dhamira ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha wanajenga vituo vitakavyo kabiliana na changamoto hiyo.
“Takwimu za mwaka 2018 zinaonesha watoto zaidi ya Mil. 2 chini ya miaka mitano wamedumaa na asilimia 43 ya watoto hao wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu ya ukuaji kutokana na kukabiliwa na viashiria mbalimbali ikiwemo utapiamlo, kukosekana kwa uhakika wa chakula, msongo wa mawazo, pamoja na utelekezaji na unyanyasaji wa watoto” amesema Waziri Gwajima, na kuongeza, “katika mwaka mmoja uliopita matukio ya kikatili yameongezeka kutoka 15,680 kwa mwaka 2019 hadi matukio 15,870 kwa mwaka 2020, aidha kuanzia mwezi Januari hadi Septemba, 2021, jumla ya matukio 6,168, yanayowahusu wasichana yakiwa 5,287 na yanayo wahusu wavulana 881. Haya ni baadhi ya matukio yaliyotolewa tolewa taarifa, lakini naamini huenda kuna matukio mengi ambayo hayakutolewa taarifa kwenye vyombo vya dola" amesisitiza Dkt Gwajima.
Katika harakati za Serikali za kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazo mkabili mtoto, mwaka 2017, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga kiasi cha shilingi 1,000 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kila mtoto ili kuwezesha kutekeleza afua za Lishe na kutokomeza udumavu na utapiamlo miongoni mwa watoto waliochini umri wa miaka mitano.
Katika hatua ya sasa, Dkt Gwajima amesema kuwa, Serikali inatarajia kujenga vituo vya mfano vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika kila kijiji/mtaa na kwenye shule za msingi nchi nzima ili kupunguza ukatili na udumavu kwa watoto ambapo Serikali na Wadau inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kipindi cha 2017/18-2021/22.
Katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima, amezitaka Wizara za kisekta, ikiwepo Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Mashirika yasiyo ya kiserikali watendaji ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri kila mmoja kwa nafasi yake kusimama kidete ili mpango huo uweze kufanikiwa.
MWISHO