Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUJA NA MTAALA WA LISHE NA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA MASHULENI NA VYUONI.

Posted on: March 12th, 2024



Na WAF - Dar Es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuna haja ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara za kisekta kuja na mtaala ambao utalenga kuelimisha jamii ya watoto na vijana balehe kuhusu lishe na afya ya uzazi kwa vijana kuanzia mashuleni hadi vyuo vikuu.

Waziri Ummy Mwalimu amesema hayo Machi 12, 2024 alipokutana na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF) Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Etleva Kadili katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu pamoja na Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikina na UNICEF wanaweza kusaidia kuboresha Huduma ya Afya ya Msingi kwa kuja na Mtaala utakaolenga kutoa elimu juu ya masuala ya lishe na Afya ya uzazi kwa vijana balehe.

"Sekta ya afya tunakusudia kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya afya, kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya. Hii itaiwezesha Tanzania kukomesha vifo vinavyoweza kuzuilika, Kuongeza upatikanaji wa bima ya matibabu ambapo Serikali inatarajia kuzindua Bima ya Afya kwa Wote na kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya milipuko na dharura". Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametoa rai kwa shirika la UNICEF kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kutambua na kubaini changamoto za Afya zinazoweza kujitokeza katika maeneo yao na kuziwaisha katika vituo vyaf kutolea huduma za afya na Kusaidia vituo vya afya kuanzisha kona za huduma za maendeleo ya awali ya watoto (ECD) katika vituo vya afya kwa ajili ya kuboresha huduma.

Kwa upande wake Etleva Kadili ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na waziri Ummy kwa uongozi mahiri katika Sekta ya Afya kusimamia kikamilifu utekelezaji na utaji wahuduma za chanjo, kundeleza mapinduzi kuboresha huduma za Mama na mtoto, kuboresha za jamii kupitia wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii.