Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ONGEZENI KASI YA UTOAJI WA HUDUMA ZA UUGUZI NA UKUNGA

Posted on: September 5th, 2024

Na WAF - Dodoma 


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Idara ya Uuguzi na Ukunga kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga pamoja na kufuatilia ubora wa kazi hizo ili mwananchi apate huduma iliyobora. 


Waziri Mhagama amesema hayo leo Septemba 5, 2024 wakati wa kikao na Idara ya Uuguzi na Ukunga kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili utendaji kazi wa Idara hiyo katika Wizara ya Afya.


“Hakuna jambo ambalo linakera unapokutana na muunguzi au mkunga anaeshindwa kutekeleza wajibu  wake kwa jambo la msingi la kutetea uhai wa mgonjwa pindi anapoitaji huduma yake.”Amesema Waziri Mhagama 


Aidha Waziri Mhagama amesema mtumishi hatakiwi kuwa na presha, anatakiwa apewe  haki zake zote za msingi ili mtumishi huyo azingatie wajibu wake wa kumhudumia mgonjwa na kuokoa maisha yake.


Awali Wakati akitoa taarifa ya Idara ya Uuguzi na Ukunga akimwakilisha  Mkurugenzi wa idara hiyo bwana Saturini Manangwa amesema idara hiyo imefanikiwa Kuimarisha ubora wa huduma za akina mama kabla, wakati na baada ya kujifungua  kwa kuanzisha huduma mwambata kwenye vyumba vya kujifungulia ambapo hadi sasa jumla ya vituo 41 vimeanzisha utoaji wa huduma hiyo 


Bwana Manangwa amesema, miongoni mwa majukumu ya idara hiyo ni pamoja na kuimarisha ubora wa huduma za Uuguzi na Ukunga katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma vya umma na binafsi, Kutoa ushauri wa kimkakati kwa Serikali kuhusu huduma za Uuguzi na Ukunga katika mfumo wa sekta ya afya.


“Majukumu yetu mengine ni kuhamasisha matumizi ya tafiti na kuwa na huduma linganifu pamoja na Kuimarisha ushirikiano na wadau wote ngazi ya Taifa, Kanda na Kimataifa, kusimamia  mafunzo mahala pa kazi kwenye huduma za Uuguzi na Ukunga.”Amesema Bw. Manangwa


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Ndg. Ismail Rumatila ambapo ameendelea kukutana na Idara mbalimbali za Wizara ya Afya kwa lengo la kutambua majukumu ya Idara pamoja na kujadili namna ya utendaji kazi wa Idara hizo.