Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ONGEZEKO LA MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WA KINYWA NA MENO LIMEZINGATIA MAHITAJI YA JAMII

Posted on: November 15th, 2024

Na WAF - Bariadi, Simiyu

Kuongezwa kwa kada ya Watalamu wa afya ya kinywa na meno katika timu ya kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia awamu ya pili kumezingatia uhitaji wa huduma hizo katika jamii.

Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bariadi Mji, Dkt. Rosemary Mushi Novemba 14, 2024 wakati akizungumzia maendeleo ya Kambi ya Madaktari Bingwa hao katika mkoa wa Simiyu.

Dkt. Mushi amesema uhitaji wa huduma za afya ya kinywa na meno ni mkubwa, licha ya Serikali kuwezesha vifaa vya kutolea huduma, lakini bado wataalamu waliopo katika vituo vya Afya vya Msingi wana uhitaji wa kupigwa msasa ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa wa afya ya Kinywa na meno.

“Kuongezwa kwa wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno kuna tija mfano kama hapa kwetu wateja wa meno ni wengi na pia mtaalamu wetu alikuwa ni ajira mpya kwahiyo siyo mzoefu sana ila tuna tumaini kwa kipindi atakachokaa karibu na mabingwa hawa hususani wa meno watamjengea uwezo na uzoefu mkubwa ili kutoa huduma bora zaidi,” amesema Dkt. Mushi.

Dkt. Mushi ameongeza pia kuwa madaktari bingwa wameweza kuhudumia wagonjwa wa afya ya kinywa na meno wengi na kutatua shida nyingi zinazowakabili wagonjwa ambapo kwa sasa kwa siku wanatibu hadi watu 10 wa kinywa na Meno.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea hawa Mabingwa na huduma za kibingwa karibu kwani wamesaidia kurahisisha uboreshaji wa huduma kwa wananchi na pia hata sisi watoa huduma kujengewa zaidi uwezo ili kuongeza ubora katika huduma zetu za Afya,” amesema Dkt. Mushi.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Dkt. Gustav Rwekaza amesema kwa siku tatu alizokuwepo kituoni hapo idadi ya wagonjwa imekuwa ikipanda kila uchwao na kwamba idadi ya wagonjwa wanaofika hapo kila siku inatosha kuonesha ni kiasi gani Serikali inagusa mahitaji ya jamii.