Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MOROGORO RRH YASISITIZWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Posted on: March 7th, 2024



Na. WAF, Morogoro
Mkurugenzi wa huduma za tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo ametoa rai kwa viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Morogoro kuendelea kutoa Huduma bora kwa wananchi ili kuleta thamani ya uwekezaji uliofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Afya

Prof. Ruggajo amesisitiza hivyo wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kuona hali ya utoaji Huduma na utekelezaji wa shughuli za hospitali hiyo.

Prof. Ruggajo amesema kuwa kila mtu akumbatie ubora wa huduma, kila mtumishi anahusika na ubora wa Huduma hivyo wakumbushane kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa wao kwa kuanzia getini anapoingia Mgonjwa ajisikie yupo sehemu ya faraja, sehemu ya huruma.

Vile vile Prof. Ruggajo amesisitiza suala la kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na maadili ya Utumishi ili kuleta ubora wa Huduma kwa wagonjwa.

"Tuheshimishe taaluma zetu kwa kufuata viapo vyetu maadili na miiko ya taaluma kwani serikali imetujali sana kwa kuwekeza vifaa vya kisasa, kusomesha wataalamu na kuboresha miundombinu ya kufanyia kazi", ameongeza Prof. Ruggajo

Aidha amesema uwekezaji mkubwa umefanyika katika miundombinu ya kutolea Huduma za afya, katika hilo tuna mshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake amewekeza zaidi ya trilioni 6.7 katika sekta ya afya.

“Katika uwekezaji huo umesaidia kutanua wigo wa upatikanaji wa Huduma za CT scan Mikoa yote, kuongezeka kwa upatikanaji wa Dawa ambapo zaidi ya bilioni 16 kila mwezi na kufanya upatikanaji wa dawa kufikia zaidi ya asilimia 90% na wananchi kwa sasa hawatembei mwendo mrefu kufata Huduma za afya”, ameeleza Prof. Ruggajo

Katika ziara yake Prof. Ruggajo amepata kukagua maendeleo ya miradi ya Jengo la Dialysis, famasi ya jamii na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) linaloendelea kukarabatiwa katika Hospitali hiyo.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Hadija Bushahu ameshukuru huduma za Afya zinaendelea kuboreka zaidi hata kwenye tiba jumuishi