Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MOROGORO KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA HOSPITALI ZOTE ZA HALMASHAURI KWA SIKU TANO

Posted on: June 3rd, 2024



Na WAF - Morogoro

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, Juni 03, 2024, amewapokea madaktari bingwa 35 ambao watatoa huduma za kibingwa katika hospitali za halmashauri za wilaya saba mkoani Morogoro kwa siku tano kuanzia Juni 03 hadi 07, 2024.

"Mpango huu kabambe wa kusogeza huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ngazi ya halmashauri utaboresha ubora wa huduma lakini pia na kupunguza vifo visivyo vya lazima," amesema Mhe. Malima.

"Nawashukuru madaktari bingwa wetu kwa mwitikio wenu wa kusaidia Watanzania wenye uhitaji wa huduma za kibingwa," amesema Mhe. Malima.

Aidha, Mhe. Malima amewahimiza Madaktari bingwa kuwajengea uwezo watoa huduma katika maeneo yao ya kazi ili kuimarisha utambuzi, matibabu, upasuaji na rufaa kwa wagonjwa wa ngazi za halmashauri.

Mhe. Malima ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza katika hospitali za wilaya zote mkoani Morogoro, ili kunufaika na ujio huu wa madaktari bingwa na ubingwa bobezi

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Urio Kusirye amewahimiza madaktari bingwa kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano wa hali ya juu na madaktari wenyeji.

Dkt. Urio amesema ujio wa madaktari Bingwa utasaidia Hospitali kuanzisha na kuimarisha wodi maalumu za watoto wachanga,hali ambayo itasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kutoka hospitali za Halmashauri.