Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MILION 800 KUGHARAMIA MATIBABU YA MACHO SIHA

Posted on: May 5th, 2025

Na WAF, KILIMANJARO

Taasisi ya Dkt. Godwin Mollel kwa kushirikiana na Mo Dewji Foundation zimetoa huduma ya bure ya matibabu ya macho kwa wananchi zaidi ya 3,000 katika Hospitali ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro zikijumuisha upasuaji wa macho, utoaji wa dawa na miwani kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa jamii, hususan kwa wenye uhitaji.

Akizungumza wakati wa kambi hiyo ya matibabu, Mei 04, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo zinazoendelea kutolewa bure.

“Huduma hii ni sehemu ya ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kiuchumi ambapo taasisi ya Dkt. Mollel na Mo Dewji zitagharamia matibabu yote bure kwa wananchi,” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel ameongeza kuwa, taasisi hizo zimeweka kambi hiyo ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi zao za kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wote nchini.