MAMA ALIYETESEKA NA UVIMBE WA KILO 15, MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAMPA TABASAMU
Posted on: October 5th, 2025
Na WAF, Nzega
Madaktari Bingwa wa Samia wanaotoa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamefanikiwa kufanya upasuaji na kutoa uvimbe wenye uzito wa kilo 15 kutoka kwa mama mwenye umri wa miaka 45 ambaye alisumbuliwa na uvimbe huo kwa miaka saba.
Akizungumzia upasuaji huo Daktari wa Bingwa wa Upasuaji Dkt. Loth Joseph, amesema mama huyo alikuwa na uvimbe ambao ulisababishwa na mayai ya uzazi kupata changamoto na kuanza kuvimba taratibu huku akitafuta huduma bila mafanikio.
"Mama huyu aliyefikishwa Hospitalini hapa akiwa na malalamiko ya kuumwa na tumbo baada ya kumfanyia vipimo tulibaini uvimbe huo ulikuwa na kilo 15 ambao ulimsumbua kwa miaka saba, hivyo ikatulazimu tumfanyie upasuaji wa haraka ili kuuondoa na sasa anaendelea vizuri," amesema Dkt. Loth.
Kabla ya kufika hospitalini hapo na kuonana na madaktari bingwa wa Rais Samia, mama huyo alitafuta huduma katika maeneo mbalimbali lakini alishindwa kutibiwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kusafiri kwenda hospitali kubwa, hivyo ikamlazimu kukaa na uvimbe katika kipindi chote hicho.
Mapema wiki hii Madaktari Bingwa wa Rais Samia wameendelea na huduma za kibingwa katika hospitali zote za wilaya za mkoa huo, ikiwa ni juhudi za Serikali kuwasogezea huduma wananchi lakini pia kuwajengea uwezo wataalam wa ngazi za wilaya.