MAFUNZO YA HUDUMA ZA DHARURA YA AJALI YAZUIA RUFAA 67 MOROGORO RRH
Posted on: October 17th, 2025
Na. WAF, Morogoro
Jumla ya rufaa za wagonjwa 67 hazikutolewa kutokana na wagonjwa hao kunufaika na huduma zinazotolewa na wahitimu wa mafunzo ya kuhudumia wagonjwa wa dharura ya ajali na kiharusi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro, ambao awali walipaswa kwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Hayo yameelezwa leo Oktoba 17 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe mkoani Morogoro, wakati akifunga mafunzo wa mwezi mmoja kwa mara ya kwanza ya kuzijengea uwezo hospitali za rufaa za mikoa kuhudumia wagonjwa wa dharura za ajali na kiharusi.
Amesema taarifa ya mafunzo hayo imeonesha kwamba jumla ya wagonjwa wa dharura 80 walionwa na wagonjwa 24 waliofanyiwa upasuaji wa dharura.
“Idadi hii ya wagonjwa walionufaika ni ishara kwamba mafunzo haya yakifanyika nchi nzima yatapelekea wananchi wengi kunufaika na kupunguza adha kwa wananchi ya gharama na muda wa matibabu,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Dkt. Shekalaghe amebainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza rufaa lakini pia kutoa rufaa zilizokuwa bora ambazo zitakuwa zimeshatibika na zinapokwenda zinakwenda kupata huduma za kibingwa bobezi.
Amempongeza Mkurugenzi wa MOI kwa kutekeleza maagizo yake ya kuleta madaktari bingwa bobezi mkoani morogoro na kujengea uwezo wataalam wa dharura na kusema matokeo ya mafunzo hayo tayari yameanza kuonekana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba , Dkt. Hamad Nyembea amesema mafunzo hayo ya awamu ya kwanza yamehusisha mikoa ya kanda ya mashariki na kwamba mkoa wa Morogoro imekuwa na historia ya ajali nyingi hivyo kujengea uwezo wataalam wa kanda hii ni kuboresha huduma za dharura za ajili na kuokoa maisha ya wananchi.
“ Jukumu la hospitali kubwa za kitaifa kama MOI ni kusaidia kuboresha huduma za afya nchini, Tukio hili linalenga kuboresha huduma za dharura za ajali ambalo linategemea sana uimara wa mifumo, rufaa zinazotolewa na kuandaliwa kabla ya kusafirishwa hivyo wamekuja wakiwa seti nzima kwenye kutoa mafunzo na wamefanya hivi ili kuwa mfano kwa taasisi zingine lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya na kuwafikia wananchi kwa urahisi,” amesema Dkt.