Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WACHAGIZA UBORA WA MIUNDOMBINU KATAVI

Posted on: May 19th, 2025

Na WAF, Katavi


Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko amesema maboresho makubwa yamefanyika katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, hivyo ujio wa madaktari bingwa unatarajiwa kuongeza ujuzi na kuimarisha uwezo wa watoa huduma katika maeneo hayo.


Mhe. Mrindoko ameyasema hayo Mei 19, 2025 wakati wa zoezi la mapokezi ya Madaktari Bingwa 34 wa fani mbalimbali za kibingwa ambao watatoa huduma katika halmashauri zote tano (5) za mkoa wa Katavi kuanzia Mei 19-24, 2025.


 “Watakapoondoka madaktari hawa, watakuwa wamewajengea uwezo namna ya kutumia vifaa tiba mbalimbali ambavyo Serikali yetu ya awamu ya sita imewekeza vyakutosha kwa ngazi za halmashauri,” amesema Mhe. Mrindoko.


“Niwahakikishie watoa huduma wote wa afya juu ya usalama katika utendaji wenu wa kazi, mazingira ya kufanyia kazi yameimarishwa na yataendelea kuboreshwa kila siku,” amesema Mhe. Mrindoko 


Akizungumza kwa niaba ya madaktari bingwa, Daktari Bingwa wa watoto, Dkt. Anna Magembe, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili  kupata huduma za kibingwa walizowasogezea.


“Tumekuja kutoa huduma za kibingwa, tuna madaktari bingwa wa watoto, magonjwa ya dharura, magonjwa ya kina mama, upasuaji na magonjwa ya ndani. Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili kufaidika na huduma hizi,” amesema Dkt. Magembe.