Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA NGUZO IMARA UIMARISHAJI HUDUMA ZA RUFAA KUTOKA NGAZI YA MSINGI

Posted on: October 21st, 2025

Na WAF-Geita

Mfumo wa rufaa wa huduma za afya mkoani Geita umeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuendeleza ujuzi na uwezo wa wataalamu wa afya ngazi ya wilaya, ambao sasa wanaweza kutoa maamuzi sahihi kwa wagonjwa wanaohitaji rufaa, sambamba na kuimarisha mawasiliano na uratibu kati ya vituo vya rufaa na ngazi hizo.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omari Sukari, leo Oktoba 20, 2025 wakati wa kuwapokea Madaktari Bingwa wa Rais Samia, kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa rufaa na ufuatiliaji wa wagonjwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya madaktari bingwa na wataalam wa afya wa ndani.

“Tumeimarisha njia ya kutambua wagonjwa wanaohitaji rufaa haraka na ushirikiano kati ya vituo vya afya, hospitali za wilaya na ya mkoa umeongezeka. Ufuatiliaji wa wagonjwa waliotibiwa kwenye kambi pia unafanyika vizuri sasa,” amesema Dkt. Sukari.

Ameongeza kuwa lengo kuu la kambi hizo si tu kutoa huduma za kibingwa, bali pia kuhamisha ujuzi kwa wataalam wa ndani ili huduma ziwe endelevu na zenye ubora zaidi hata baada ya madaktari bingwa kuondoka.

“Tunataka madaktari wetu wa ndani wajifunze na kuwa na uwezo wa kutoa huduma bora za kibingwa. Hilo ndilo litakalohakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa ufanisi,” amesisitiza Dkt. Sukari.

Kwa upande wake, mratibu wa Madaktari Bingwa kutoka Wizara ya Afya, Bi. Paskalina Mahu, amewataka madaktari hao kutumia muda wao kufanya kazi kwa ushirikiano na weledi, ili kufanikisha malengo ya kambi hiyo kama yalivyokusudiwa na Serikali.

“Tunatarajia kila daktari atafanya kazi kwa weledi, kushirikiana na wenzao wa ndani, na kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wengi zaidi,” amesema Bi. Mahu.

Kambi ya Madaktari Bingwa ya Mama Samia imekuwa ikitekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, kuimarisha mifumo ya rufaa na kuongeza ujuzi kwa watumishi wa afya wa ndani.