Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAAFISA AFYA MIPAKANI WAFANYA MAFUNZO KWA VITENDO

Posted on: October 23rd, 2025

Na WAF, Dar es Salaam

Maafisa Afya wa Mipaka ya Bandari wamefanya mafunzo kwa njia ya vitendo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kukagua moja ya meli ya kigeni ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mafunzo ambayo awali waliyapata kwa njia ya nadharia.

Mkuu wa huduma za Afya mipakani Wizara ya Afya, Dkt. Amour Selemani amesema hayo leo Oktoba 22, 2025 jijini Dar es Salaam akiwa na wataalam hao katika mafunzo Bandarini jijini Dar es Salaam.

Dkt. Amour amesema maeneo wanayofanya ukaguzi ndani ya meli ni mazingira yanayoandaliwa chakula ndani ya meli, vyumba vya kulala, sehemu ya kutolea huduma ya kwanza, mazingira ya chumba cha uendeshaji mitambo, upimaji wa afya kwa wahudumu wa meli na sehemu za kuhifadhi taka pamoja na kujua meli inatoka nchi gani.

Akizungmza wakati wa zoezi hilo Afisa Afya Bandari ya Mwanza, Bi. Leila Miraji amesema mafunzo hayo yanayoendelea tayari yamewajengea uwezo wa kujua vigezo vinavyotumika kimataifa katika ukaguzi wa meli na utoaji wa vyeti mara baada ya ukaguzi wa meli husika.

Naye Afisa Ufuatiliaji wa Magonjwa Dkt. ya Mlipuko kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Bw. George Kauki amesema shirika hilo linashirikiana na Serikali ya Tanzania ili kutambua namna ya kujikinga na kudhibiti magonjwa mbalimbali sambamba na kufuatilia kanuni za kimataifa (IHR 2005) inayo zitaka nchi wanachama wa shirika hilo kuzuia magonjwa yanayoweza kusambaa kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Dkt. Kauki ameongeza kuwa WHO kupitia Uimarishaji Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko (Pandemic Fund) litawezesha ununuzi wa vifaa muhimu vya kutambua na kudhibiti magonjwa ambayo yanaweza kuenezwa kupitia mipaka ya bandari na kuenea katika nchi nyingine.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na WHO imeandaa mafunzo hayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa hitaji la wataalam wenye uwezo wa kutambua na kudhibiti magonjwa ya mlipuko na Uhimarishaji Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko ujulikanao Pandemic Fund.