Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA RUFAA MKOA MTWARA KUANZA KUTUMIKA APRILI 1, 2024

Posted on: March 11th, 2024



Na: WAF, Mtwara

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ameagiza kukamilika kwa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Machi 31, 2024 na kuanza kutumika ifikapo Aprili 1, 2024 ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Dkt. Magembe ameyasema hayo leo Machi 11, 2024 akiwa katika ziara Mkoani Mtwara kwa ajili ya kukagua miradi ya ujenzi wa hospitali, vifaa, ubora wa huduma na kuzungumza na watumishi juu ya maadili na miongozo ya kazi.

“Hakikisheni jengo hili la mama na mtoto mpaka Machi 31 liwe limekamilika na ifikapo Aprili huduma zianze kutolewa katika jengo hili, watoke kule kwa zamani waje huku kwenye jengo jipya ambako miundombinu ya kutolea huduma imeboreshwa”. Amesema Dkt. Magembe

Dkt. Magembe amesisitiza kwamba kukamilika kwa jengo hilo kutarahisisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

Hata hivyo Dkt. Magembe ameagiza mchanganuo wa vifaa vya ujenzi na gharama za ufundi za kumalizia ujenzi wa jengo la Dharura (EMD) kuandaliwa haraka ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kukamilisha ujenzi huo kabla ya Julai 2024.

Aidha, Dkt. Magembe ameagiza mchakato wa kufunga awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) uanze maramoja na mchakato wa kutafuta Mkandarasi mpya atakaye endelea na awamu ya pili ya ujenzi uanze ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo la OPD.

Dkt. Magembe ameyasema hayo baada ya jengo hilo kusimama kwa muda mrefu bila ujenzi kuendelea.