Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA KIBINGWA ZAENDELEA KATIKA HALMASHAURI 08 KIGOMA

Posted on: June 10th, 2024


Na WAF – Kigoma

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amewataka Madaktari Bingwa wa Rais Samia kufanya kazi kwa upendo uadilifu, weledi na utu katika utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafundisha wataalamu watakaofanya nao kazi katika vituo walivyopangiwa

Mhe, Andengenye ameyasema hayo mapema Juni 10, 2024, katika uzinduzi wa kambi za Matibabu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika ngazi ya Wilaya iliyofanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Ujiji mkoani Kigoma ambapo Madaktari hao watatoa huduma za Uchunguzi na matibabu ya kibingwa katika Hospitali zote 8 za Wilaya zilizo Mkoani Kigoma.

Mkuu wa mkoa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuijali Sekta ya Afya nchini katika kuanzisha huduma mbalimbali zikiwemo za Kibingwa na Ubingwa Bobezi ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba, uboreshaji wa miundombinu pamoja na huduma za vipimo.

“Naishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu huduma mkoba hizi kuendelea katika ngazi ya Halmashauri, tulianza na Kambi za Matibabu ya Madaktari Bingwa Ngazi ya Mkoa na sasa rasmi tumehamia kwenye Hospitali za Wilaya”. Amesema Mhe. Andengenye.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba amebainisha kuwa kambi hizi zitasaidia wananchi wengi kuondokana na changamoto za kiafya walizokua nazo na kuwapunguzia changamoto ya matibabu katika wilaya husika.