HUDUMA ZA KIBINGWA 'ENT', KUSAFISHA DAMU KUPATIKANA HOSPITALI MT. FRANSISCO
Posted on: April 30th, 2025
Na WAF - Kilombero, Morogoro
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amezindua huduma za kibingwa na kibobezi za Masikio, Pua, Koo (ENT) pamoja na uchujaji damu (Homodialysis Unit) katika Hospitali ya Rufaa ya MT. Fransisco iliyopo Ifakara, Kilombero mkoani Morogoro.
Waziri Mhagama amezindua huduma hizo leo Aprili 30, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya MT. Fransisco ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi, kisha kuzungumza na watumishi pamoja na viongozi wa hospitali hiyo.
Waziri Mhagama amesema hospitali hiyo ya Mt. Fransis inayotimiza miaka 100 ndio kimbilio la huduma za tiba kwenye ukanda huo wa bonde la mto Kilombero.
Waziri Mhagama amesema katika Hospitali hiyo ya St. Francisco, yenye watumishi 417 na kati yao watumishi 206 ni watumishi walioajiriwa na Serikali kupitia Halmashauri pamoja na Wizara ya Afya.
"Hii inaonesha dhahiri kuwa, Serikali ya awamu ya Sita (6) chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha nia ya dhati ya kushirikiana na sekta binafsi na Taasisi za dini kuimarisha ubora wa huduma katika sekta ya afya na kumfikia kila mwananchi," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, Kutokana na ushirikiano huo, asilimia 80 ya wananchi kwa sasa wanazifikia huduma za afya ndani ya kilometa tano (5).
"Niwahakikishie Serikali inayosimamiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa ushirikiano katika kuboresha huduma za afya kwa sekta binafsi ikiwemo Taasisi za kidini." amefafanua Mhe. Mhagama.
Pia, Waziri Mhagama amesema Serikali ya awamu ya Sita imeahidi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zenye kujali utu, huku akisisitiza kuendelea kutilia mkazo ahadi hiyo ya Serikali kwa wananchi.
"Kila mtumishi anakiapo chake ninawaomba muishi kwenye viapo vyenu, kwani kuna baadhi ya watumishi wanakiuka viapo vyao, " amesisitiza Mhe. Mhagama.
Amesema kuwa baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia lugha chafu, watoro na wenye dharau hivyo wanatakiwa kubadilika kwa kuwajibika kwenye majukumu yao iliwa ni pamoja na kutii na kuheshimu maelekezo na maagizo ya viongozi.
Kwa upande mwingine Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kuuagiza mfuko wa bima ya afya (NHIF) kulipa fedha za hospitali kwa wakati ili kuziwesha hospitali hizo kujiendesha ikiwemo kulipa posho za wataalamwa afya (oncall alawance) ili kuwepo na dhamira ya kuonesha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi.