Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HALMASHAURI 112 KATI YA 119 NCHINI HAZINA MAAMBUKIZI MAPYA YA MATENDE NA MABUSHA

Posted on: March 12th, 2024



Na. WAF - Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesitisha kampeni ya umezeshaji wa kingatiba za ugonjwa wa Mabusha na Matende katika Halmashauri ya Jijini la Da Es Salaam, Manispaa ya Temeke na Kata 10 za Manispaa ya Kinondoni ambazo hazina maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 12, 2024 wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya hatua zilizofikiwa za kutokomeza ugonjwa wa Matende na Mabusha nchini hususan katika Mkoa wa Dar Es Salaam.

“Serikali kwa kushirikiana na Wadau tumeweza kudhibiti ugonjwa huu katika Halmashauri 112 kati ya 119 a kubakiwa na Halmashauri 7 ambapo mafanikio hayo yamechangiwa na kampeni za utoaji elimu na umezaji kingatiba za ugonjwa huo zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri @ummymwalimu amesema bado kuna baadhi ya Halmashauri ambazo bado zina maambukizi mapya ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na Pangani, Mafia, Kinondoni, Kilwa, Lindi Manispaa, Mtama na Mtwara Mikindani ambapo kwa ujumla kata hizo zina wakazi 1,203,359.

“Natoa rai kwa wakazi wa maeneo hayo ambayo bado kuna maambukizi ya ugonjwa huu kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kwenye kampeni za kingatiba ya ugonjwa wa Matende na Mabusha zitakazoendelea kufanyika katika maeneo yao ili kuweza kutokomeza maambukizi maya va ugoniwa huu.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, Kigamboni na Ubungo hazina maambukizi mapya kwa kipindi cha miaka sita baada ya kusitisha umezaji wa kingatiba huzo hatua iliyowezesha watu milioni 3.7 kuokolewa katika hatari ya kupata maambukizi mapya jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali Afya za Watanzania ambapo amewezesha upatikanaji wa fedha pamoja na vifaa katika kufikia mafanikio hayo.

Kwa upande wake, Mratibu Udhibiti wa Ugonjwa wa Matende na Mabusha Wizara ya Afya, Dkt. Faraja Lyamuya amesema sababu zinazochangia maambukizi mapya katika baadhi ya maeneo ni jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha pamoja na kuhamahama hatua inayosababisha kutoshiriki kikamilifu katika umezaji wa kingatiba.