Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. SHEKALAGHE AFANYA ZIARA KUKAGUA UTAYARI WA MAJENGO MAPYA HOSPITALI YA MKOA LINDI

Posted on: November 29th, 2025

Na WAF, Lindi & Mtwara

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amefanya ziara ya kukagua hatua iliyofikia ya ukamilishaji ujenzi wa majengo mapya ya Hospitali ya Mkoa wa Lindi (Sokoine) ili kuanza maandalizi ya kuhamia kwenye majengo mapya.

Akiwa katika majengo mapya ya hospitali hiyo Novemba 26, 2025 mkoani Lindi, Dkt. Shekalaghe amefanya majadiliano na wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, ambao kwa pamoja wameridhika kwa hatua iliyofikiwa hivyo kuona kuwa kuna haja ya kuanzisha huduma katika majengo mapya kutokana na kukamilika kwa miundombinu na huduma zote muhimu zinazohitajika.

Aidha, amesema hatua hiyo iliyofikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo imetoa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo mpya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya bora kwa wananchi wa Lindi na ukanda wa kusini kwa ujumla.

Akiwa mkoani Mtwara ikiwa ni muendelezo wa ziara yake siku hiyo hiyo, Dkt. Shekalaghe amewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kuendelea kutoa huduma bora zenye kuzingatia uzalendo, viapo vya maadili na miiko ya taaluma zao.

Dkt. Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kutumia lugha ya staha kwa wananchi wanaofika kupata huduma.

“Kila mmoja afanye jukumu lake, kuanzia mlinzi anayewapokea wagonjwa getini, mfanya usafi, wauguzi hadi madaktari. Tunapomhudumia mgonjwa sisi sote ni wamoja. Tufanye kazi kwa ushirikiano,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Ameongeza kuwa watumishi wa afya wanapaswa kuwa faraja kwa wananchi wanaowahudumia na kujitahidi wawe na tabasamu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni ibada na baraka kwa jamii.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amewataka viongozi wa hospitali kote nchini kuwajali na kuwathamini watumishi wao ili kujenga mazingira bora ya kazi, yenye upendo na mshikamano, hatua itakayowezesha kuboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa wananchi.