SHIRIKIANENI KUOKOA MAISHA YA WATOTO WACHANGA AFRIKA
Posted on: March 2nd, 2026Na Aisha Swahibu, WAF – Mwanza
Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Prof. Mohammed Janabi, ametoa wito kwa serikali, wadau wa sekta ya afya na jamii kwa ujumla kuimarisha ushirikiano ili kupunguza vifo vya watoto wachanga barani Afrika.
Akizungumza Februari 28, 2026, wakati wa uzinduzi wa wodi ya watoto wachanga wagonjwa na njiti (NCU) katika Hospitali ya Rufaa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, iliyopo mkoani Mwanza , Prof. Janabi amesema tatizo la vifo vya watoto wachanga bado ni kubwa.
Prof. Janabi amesema kuwa takwimu za WHO zinaonesha takribani watoto wachanga milioni moja hufariki kila mwaka katika miezi ya mwanzo baada ya kuzaliwa katika Kanda ya Afrika, hali inayohitaji hatua za haraka na za pamoja.
Prof. Janabi amesisitiza umuhimu wa kujenga na kuimarisha wodi maalum za NCU katika hospitali mbalimbali huku akitaka haja ya kuongeza mafunzo kwa watoa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu ufuatiliaji wa afya ya mama na mtoto hata baada ya kuruhusiwa hospitalini.
Prof. Janabi amesema uzinduzi wa wodi hiyo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo, taasisi za dini na jamii ili kupunguza vifo vya mama na watoto na kuwataka wananchi na watumishi wa afya kutunza miundombinu na vifaa vilivyowekwa.
Aidha, amepongeza Tanzania kwa mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kubainisha kuwa, vifo hivyo vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, kufuatia utekelezaji wa miongozo ya WHO.
Prof. Janabi ameahid kuwa, WHO itaendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.