Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

Posted on: November 25th, 2025

Na WAF – Dodoma


Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno nchini, ikiwa ni pamoja na  upatikanaji wa takwimu sahihi za huduma hizo. 


Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 24, 2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Tiba,  Dkt. Hemed Nyembea kutoka Wizara ya Afya, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Waratibu wa Afya ya Meno wa mikoa pamoja na wadau wa huduma ya meno kilichofanyika mkoani Dodoma.


“Lengo la kikao hiki ni kujadili namna ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya meno,  uongozi na usimamizi katika huduma hii,” amesema Dkt. Nyembea.


Ameongeza kuwa hata kama kutakuwa na miundombinu, vifaa na vifaa tiba vya kutosha, bila kusimamia ubora wa huduma juhudi hizo hazitakuwa na tija, akisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha usimamizi madhubuti wa ubora wa huduma za afya ya kinywa na meno ili kufikia malengo waliyojiwekea.


Aidha, Dkt. Nyembea amesema rasilimali watu katika huduma ya meno zinaendelea kuongezeka, huku Serikali ikitoa vibali vya ajira na kuboresha mazingira ya utoaji huduma. Pia, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarika na kuongeza ufanisi katika vituo vya afya.


Ameeleza kuwa tathmini iliyofanyika katika hospitali mbalimbali imeonesha uwekezaji uliofanywa umeleta maboresho makubwa katika utoaji wa huduma.


Kwa upande wake, Dkt. Baraka Nzobo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Kinywa na Meno, amesema tathmini hiyo imeonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na uwekezaji wa Serikali na wadau katika huduma ya meno.


Ameongeza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Mpango Kazi wa Huduma za Meno, ambao utaongoza utekelezaji wa afua na maboresho katika ngazi zote za mikoa.