HUDUMA YA KANGAROO 'MOTHER CARE' IFIKISHENI NGAZI YA MSINGI
Posted on: March 14th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, ametoa rai kwa Serikali kupeleka huduma za Kangaroo Mother Care (Huduma ya Malezi ya Mtoto kwa Njia ya Kangaroo) hadi ngazi ya msingi ili kuendelea kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini.
Dkt. Lukumay ameyasema hayo leo Machi 12, 2026 wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kutembelea na kukagua uimarishaji wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, jijini Dar es Salaam.
Amesema huduma ya Kangaroo Mother Care ni muhimu kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au wenye uzito mdogo kwa kuwa inasaidia kudhibiti joto la mwili wa mtoto kwa kumweka kifua kwa kifua na mama, kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto pamoja na kuongeza nafasi ya mtoto kuishi.
Aidha, amesema huduma hiyo pia huchangia kuongeza uwezekano wa mtoto kunyonya maziwa ya mama kikamilifu, kupunguza hatari ya maambukizi na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga.
“Ni muhimu kuhakikisha huduma hizi zinapatikana ngazi ya vituo vya afya na zahanati ili watoto wanaozaliwa njiti au wenye uzito mdogo waweze kupata huduma mapema bila kulazimika kusafirishwa umbali mrefu,” amesema Dkt. Lukumay.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya inayoongozwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo huduma ya malezi ya mtoto kwa njia ya Kangaroo.
Dkt. Samizi amesema katika utekelezaji wa huduma hiyo, pamoja na mama wa mtoto, baba au mlezi mwingine (surrogate)pia anaweza kushiriki katika kutoa huduma hiyo kwa kumweka mtoto kifua kwa kifua ili kusaidia kudhibiti joto la mwili wa mtoto na kuimarisha malezi ya karibu kwa watoto wanaozaliwa njiti au wenye uzito mdogo ambapo huduma hii inafanyika katika hospitali ya amana.
Amesema jumla ya wodi 362 zinatoa huduma za watoto wachanga ikiwemo huduma ya malezi ya mtoto kwa njia ya Kangaroo, huku Serikali ikiweka lengo la kufikisha wodi 580 zinazotoa huduma hiyo nchini.