TANZANIA KUENDELEA KUTUMIA TAKWIMU ZA KITAIFA NA KIMATAIFA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: November 25th, 2025Na WAF - Istanbul, Uturuki
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewawahakikishia wadau wa Sekta ya Afya kuendelea kutumia matokeo ya tafiti, takwimu sahihi na ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kulinda afya za wanawake na watoto.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Novemba 25, 2025 wakati akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Kisayansi la uzinduzi wa mradi wa utafiti wa kuzuia Magonjwa Yasiyoambukiza kwa wajawazito na watoto wachanga linalofanyika mjini Istanbul, Uturuki.
"Niwahakikishie tutaendelea kutumia matokeo ya tafiti, takwimu sahihi na ushirikiano wa Kimataifa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwakuwa Serikali yetu imedhamiria kulinda afya ya wanawake na watoto, kuimarisha takwimu za afya na kukuza ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa kwa manufaa ya Watanzania," amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe amesema juhudi zinazoendelea ili kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ni pamoja na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu kupitia DHIS2 na EMR, kuimarisha mfumo wa MPDSR katika kufuatilia na kuripoti vifo vya mama, kuongeza sehemu za kupokea taarifa za ulemavu na changamoto za kimaumbile kwenye vitabu vya MTUHA.
"Pamoja na kuboresha usajili wa taarifa za wasichana walio chini ya miaka 18 ili kuruhusu ufuatiliaji wa huduma wakati wa ujauzito, mweleko wa Serikali ni kukusanya takwimu za magonjwa kama Hepatitis B kwa watoto wachanga ili kumaliza maradhi matatu makuu ya kuambukiza kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo ni VVU, homa ya ini na kaswende," amesema Dkt. Magembe.
"Nitumie nafasi hii kuwakumbusha na kuwasisitiza wadau wote kuwa kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuboresha mifumo ya taarifa za Afya iliyopo hasa kwenye Afya ya msingi ambapo mfumo unaotumika kwa sasa ni GOTHOMIS. Tutakuwa tayari kuongeza taarifa za nyongeza kama zinahitajika na sio kuanzisha mifumo mipya ya kukusanya takwimu" alisistiza Dr Magembe.
Pia Dkt. Magembe amewashukuru wadau wote wakiwemo KCRI na Chuo Kikuu Cork cha nchini Ireland kwa utayari wao kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuboresha huduma za Afya hasa kuimarisha mifumo na kupata takwimu nzuri zenye uhakika na ambazo zitaiongoza Serikali katika kupanga mipango na kutenga rasilimali za afua mbalimbali za afya.