TOENI USHAURI MADHUBUTI ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA YA MACHO KWA WANANCHI – DKT. UBUGUYU
Posted on: November 29th, 2025Na WAF, Morogoro
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Magonjwa Yasiyoambukiza, Dkt. Omary Ubuguyu, amewataka wajumbe wa kikao kazi cha Kamati ya Afya ya Macho kujadiliana kwa kina, kutoa maoni na ushauri kwa Wizara ya Afya ili kuendelea kutoa huduma bora za macho kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo, Novemba 28, 2025, katika kikao kazi kilichopangwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, kilichohusisha Wizara na wadau wa sekta ya macho.
“Kikao hiki ni muhimu naamini ni nafasi nzuri ya kuendesha mijadala mbalimbali juu ya namna ya kuongeza huduma za matibabu ya macho na kushirikiana na wadau wetu,” amesema Dkt. Ubuguyu.
Dkt. Ubuguyu ameongeza kuwa magonjwa yanayohusiana na macho ni miongoni mwa magonjwa kumi yanayowasumbua zaidi Watanzania. Utoaji wa wataalam wa macho unaendelea kuongezeka, jambo linalosaidia kufikia idadi kubwa ya wagonjwa kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Dkt. Ubuguyu amesema Serikali, kwa kushirikiana na wadau, imeendelea kuongeza wataalam pamoja na vifaa katika vituo vya ngazi mbalimbali, hivyo kuwezesha matibabu ya wagonjwa wa macho kufanyika kwa usahihi.
Dkt. Ubuguyu amesema tunatambua mchango mkubwa wa wadau katika kutoa huduma hizi za matibabu ya macho katika kambi mbalimbali zinazofanyika nchini. Wengi wa wananchi wanahudhuria kambi hizi, jambo linaloonyesha kuwa mahitaji bado ni makubwa katika jamii.
Kwa upande wake, Programu Meneja kutoka Shirika la Kimataifa la Hellen Keller, Bw. Athuman Tawakal ameeleza kuwa wadau wanashirikiana kwa karibu na Serikali katika kutoa huduma, elimu, na kuhakikisha kuwa huduma za macho zinapatikana kwa wananchi kwa ufanisi na kwa usawa.