SHILINGI BILIONI 17 KUBORESHA HUDUMA ZA KINYWA NA MENO NCHINI
Posted on: November 28th, 2025
Na WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewekeza Shilingi za kitanzania Bilioni 17 ambazo zimetumika kuboresha vifaa vinavyohitajika kwenye kutoa huduma za kinywa na meno nchini.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 26, jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ahmad Makuwani alipo muwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe kwenye kongamano la 40 la Kisayansi na mkutano Mkuu wa wataalam wa Afya ya kinywa na meno Tanzania (TDA).
Amesema, kupitia uwekezaji huo wa vifaa tiba kwaajili ya huduma za meno na uwepo wa madaktari bingwa waliowafikia wananchi kupitia huduma za mkoba zimesaidia wananchi kuepukana na adha ya kupoteza meno kwa kiasi kikubwa au kupata madhara zaidi
“ Hatua hii imeongeza ubora wa huduma na kuwawezesha madaktari bingwa kuwafikia wananchi kupitia huduma za mkoba, jambo ambalo limechangia kupunguza hatari ya kung’olewa meno au kupata madhara makubwa ya kiafya,” amesema Dkt. Makuwani.
Naye Mkurgenzi Msaidizi Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya Dkt. Baraka Nzobo amewataka wananchi kujitokeza kwenye huduma mbalimbali zanazotolewa na mabingwa wa Afya na meno ili kutimiza dhana ya Wizara ya Afya ya kuondoa tatizo la mapengo au kibogoyo kwa kila mwananchi.
“Nawaomba wananchi wajitokeze kutumia huduma zetu za kitaalam , ili kutimiza dhamira ya Wizara ya Afya ya kuhakikisha kila Mtanzania anaepukana na tatizo la mapengo au kibogoyo maana kumekuwa na dhana mzee lazima ameng'oa meno mawili au matatu jambo ambalo sio kweli,” amesema Dkt. Nzobo.
Maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni 'Kuwezesha Ubunifu Wa Kiteknolojia Kukuza Afya Ya Kinywa Na Meno Tanzania' hufanyika kwa wiki nzima ambapo licha ya kufunguliwa kwenye mkoa mmoja unaochaguliwa, bado wananchi wananufaika nchi nzima kwa kukutana na madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno na kupatiwa matibabu.