UIMARISHAJI HUDUMA ZA AFYA, MWANAMKE KUTOTAABIKA- RC SINYAMULE
Posted on: March 8th, 2026Na, WAF - DODOMA
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha afya ngazi ya msingi hadi taifa ili kuhakikisha jamii hususan ni wanawake wanapata huduma bora za afya na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga.
Akizungumza leo Machi 8, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Sinyamule, amesema serikali imeweka mkazo wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ili wanawake wasilazimike kutembea umbali mrefu kusaka huduma.
“Serikali yetu chini ya Rais Samia imeendelea kumuinua mwanamke kupitia sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya ili kuhakikisha wanawake wanapata huduma za matibabu karibu na maeneo yao na kupunguza vifo vya mama na mtoto,” amesema Mhe. Sinyamule.
Mhe. Senyamule amezema, serikali inaendelea kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata ujumuishi katika fursa za kijamii kuelekea mwaka 2050, ikiwemo, elimu na fursa za kazi.
“Sisi wanawake si dhaifu wala wanyonge. Tukiamua kusimama hakuna anayeweza kuzuia maendeleo ya Tanzania,” amesema RC Senyamule.
Aidha, amewahimiza wanawake kuwa jasiri, kuvuka vikwazo vya kijamii na kuwa na uthubutu wa kushiriki kwenye nafasi za uongozi.
“Tunaye kiongozi jasiri anaye iongoza nchi. Uongozi wake umetambulika ndani na nje ya nchi kutokana na mambo makubwa anayoyafanya. Hili linadhihirishwa na tuzo mbalimbali alizopata, ikiwemo Goalkeeper Award kwa juhudi zake katika kupunguza vifo vya mama na watoto,” amesema Mhe. Sinyamule.
Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo: "Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050."