Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI AWATAKA MADIWANI KIBONDO KUHAMASISHA BIMA YA AFYA

Posted on: September 14th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Kibondo, Kigoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Jimbo la Muhambwe, kuichukua agenda ya bima ya afya na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima hiyo ili kuwawezesha kupata huduma za afya na kupunguza gharama za matibabu wanazokutana nazo.

Dkt. Samizi amesema hayo leo Septemba 14, 2026 akiwa wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, katika ziara yake ya kikazi Jimbo la Muhambwe, ambapo amesema Serikali imewalipia zaidi ya kaya 276,000 na kutoa Shilingi bilioni 48 ili kaya hizo ziweze kunufaika na huduma za bima ya afya kwa wote.

Amesema ushiriki wa viongozi wa Serikali za Mitaa, wakiwemo Madiwani, ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kuwa na bima ya afya na kuchukua hatua za kujiunga, kwa kuwa bima hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama.

“Tunataka Madiwani muichukue agenda hii ya bima ya afya kuwa agenda yenu, muwahimize wananchi kujiunga na bima ya afya ili pale wanapohitaji huduma waweze kupata matibabu bila gharama kubwa,” amesema Dkt. Samizi.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekusudia kuweka tabasamu kwa wananchi kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na kwa wakati.

Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi, ikiwemo kuanza uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa dawa nchini ili kuongeza upatikanaji wa dawa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi na hatimaye kuchangia kupunguza gharama za dawa na matibabu kwa wananchi, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

Dkt. Samizi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, huku akiwataka viongozi katika ngazi zote kushirikiana katika utekelezaji wa ajenda hiyo kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata hudum